Thursday, 22 June 2017

Treni za kasi zaidi Dar zaja, Mbagala, B’moyo kupata reli

KATIKA kuhakikisha inaboresha usafiri wa treni jijini Dar es Salaam, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) inakusudia kufanya mapinduzi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwa na treni za kasi zitakazotumia muda mfupi zaidi.


Aidha, inakusudia kupanua mtandao wake wa reli, ikiwamo ya kutoka Mbagala kwenda katikati ya Jiji na pia kutoka katikati ya Jiji hadi Bagamoyo. Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Masanja Kadogosa alipokuwa anazungumza na gazeti hili kuhusiana na changamoto mbalimbali zinazoukabili usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwamo msongamano kupita kiasi wa abiria wa treni inayofanya safari zake kati ya Pugu na Stesheni.
Alisema wanatambua changamoto wanazokumbana nazo abiria wanaotumia usafiri huo, lakini wako katika mikakati ya kuboresha usafiri huo hatua kwa hatua. Msongamano Alisema mkakati wa kukabili hali hiyo upo, lakini ufanyiwa usanifu na kama ukikamilika, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa abiria wanaotumia usafiri huo.
Alifafanua kuwa mkakati huo unalenga kuleta treni ambazo badala ya kutumia dakika 45 za sasa kutoka Stesheni hadi Pugu, zitatumia dakika 25 pekee, hatua ambayo itamwezesha abiria kusubiri treni nyingine endapo ataona imejaa.
Alisema wakati wakijipanga, wamefanikiwa kuondoa changamoto ya vumbi katika reli, kwani kampuni imetandika reli yenye urefu wa kilometa 20, hivyo kuondoa changamoto hiyo ambayo ilikuwa kero kwa abiria.
Aliongeza kuwa, mafundi pia wameendelea kuboresha mambo mengine katika mabehewa ikiwa ni pamoja na kufunga feni ili kuwaondolea adha ya joto. Alisema mkakati huo wa kudumu utahusisha uanzishwaji wa safari kati ya Bagamoyo hadi Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege hadi mjini, Mbagala hadi mjini pamoja na njia nyingine kwa kadri watakavyoona inafaa.
“Hata kama kuna mabasi ya mwendo kasi, zote zinaweza kufanya kazi na kusiwe na mwingine kwa sababu treni inabeba abiria wengi kwa wakati mmoja, lakini mabasi yanachukua watu wachache, huu mkakati kwa sasa uko katika designing (usanifu) na tunaendelea nao,” alisema.
Awali mwandishi wa habari hizi, alisafiri na treni hiyo na kujione kero mbalimbali wanazokumbana nazo abiria, ambapo kwa nyakati tofauti abiria hao waliitaka kampuni hiyo kuhakikisha inatatua changamoto hiyo.
Mkazi wa Tabata Kinyererezi ambaye anatumia usafiri huo, Mwanaamina Juma alisema changamoto ziko nyingi lakini changamoto kubwa ni treni hiyo kujaza abiria kupita kiasi jambo ambalo ni hatari.
“Unakuta behewa linajaza kupita kiasi hadi hewa inakosekana na madirisha yenyewe madogo na feni hazifanyi kazi, kwa kweli hii ni hatari watu wanaweza kuambukizana hata magonjwa,” alisema.
Naye Samson Said mkazi wa Mombasa alisema, licha ya kwamba treni hiyo ni usafiri wa wote, lakini anakosoa utaratibu wa abiria kukatishwa tiketi ingawa si wote wanaosafiri kwani tiketi zinakatwa kuzidi uwezo wa treni, hivyo kuwapotezea muda abiria kwa kulazimika kusubiri treni irudi ama kutoka Pugu au Stesheni ndipo aanze tena safari.
Kwa kawaida, safari kati ya vituo hivyo huchukua kati ya saa mbili. Abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Suzan Alponce alisema, pamoja na kwamba maeneo mengi hayana sehemu za kupumzikia abiria, lakini pia hakuna taa hali ambayo inawashawishi vibaka kufanya uhalifu.
Alisema, ikiwa mtu anarudi nyakati za usiku kwanza ni vigumu kwa yeye kutambua mahali anaposhuka, lakini pia wezi wanaweza wakatumia mwanya huo kupora mali za abiria.
“Japo mnashuka wengi, lakini ikitokea umebaki nyuma peke yako unaweza ukakabwa na hata wakakudhuru kwa sababu ni giza. Lakini pia kuna baadhi ya vituo mfano Banana kuna madimbwi mvua ikinyesha ni tabu tupu,” alisema.
Usafiri huo wa treni umekuwa mkombozi kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam hasa wakazi wa maeneo ya Tabata, Mabibo na Ubungo kwa treni la Ubungo na wakazi wa Vingunguti, Ukonga, Gongo la Mboto na maeneo mengine yanakopita treni hiyo

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!