Sunday 8 February 2015

TANZANIA INA ZIADA YA TANI MILIONI 3.2 ZA CHAKULA

unnamedkay1
Hussein Makame-MAELEZO,Dodoma
TANZANIA ina ziada ya tani Milioni 3.2 za chakula kutokana na uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa 2013/2014 kufikia jumla ya tani Milioni 16.0 wakati makadirio ya mahitaji ya chakula kwa mwaka 2014/2015 ni tani Milioni 12.8.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akisoma hotuba ya kuahirisha mkutano wa 18 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliokaa kwa siku 12 mjini Dodoma.
“Tathmini ya awali ya uzalishaji wa mazao ya chakula nchini hadi Mwezi Septemba mwaka 2014 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa kilimo 2013/2014 ulifikia jumla ya Tani Milioni 16.0 zikiwemo Tani Milioni 9.8 za mazao ya nafaka na Tani Milioni 6.2 za mazao yasiyo ya nafaka” alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Alisema kutokana na hali hiyo, Tanzania imeweza kujitosheelza kwa chakula kwa asilimia 125, hali iliyomfanya kuwapongeza wakulima kwa kuitikia wito wa Serikali wa Mpango wa Kilimo Kwanza ambao umeongeza tija katika uzalishaji.
Kwa upande wa utekelezaji wa maagizoya ujenzi wa maabara nchini, Waziri Mkuu Pinda aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya, mameya, wenyeviti na wakurugenzi watendaji wa halmashauri za wialaya na miji nchini kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa.
Alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, mkoa wa Njombe ambao ulifanikiwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya maabara kwa asilimia 96 ya shule za sekondari zilizopo mkoani humo huku mkoa wa Ruvuma na Morogoro ukikamilisha ujenzi huo kwa asilimia 81, 53 mtawalia.

Aliitaka mikoa ambayo haijakamilisha ujenzi huo kuhakikisha inakamiliasha hadi kufikia mwezi Juni, 2015 kama Rais Jakaya Kikwete alivyoagiza.
Akizungumzia utekelezaji wa Mradi wa REA wa upatikanaji wa nishati ya umeme vijijini, Waziri Mkuu alisema idadi ya Watanzania waliounganishwia umeme imeongezeka kutoka asilimia 2.5 kwa mwaka 2007 hadi asilimia 18.4 kwa mwaka 2010 na kufikia asilimia 24 kwa mwaka 2014.
Katika Mkutano huo wa 18 wa Bunge la Jamhuri, jumla ya maswali 122 ya msingi na 313 ya ngongeza yaliulizwa na wabunge na maswali 15 ya msingi kwa Waziri Mkuu na nyongeza 13 yaliulizwa.
Mkutano huo umeahirishwa hadi Machi 17 mwaka huu ambapo Bunge hilo litakutana tena katika Mkutano wa 19.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!