Sunday 8 February 2015

WAUMINI WA DINI ZOTE LIOMBEENI TAIFA AMANI-DK- BILAL


Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amewataka waumini wa dini zote nchini kuiombea Tanzania amani wakati ikiingia kwenye upigaji wa kura ya maoni ya katiba mpya na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.



Bilal alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe za kanisa hilo ambapo pamoja na mambo mengine amewakumbusha waumini kuwa wadumishe amani na utulivu.

“Sote ni mashuhuda tunaona changamoto za majirani zetu wanaopigana vita na kufikia kukimbia nchi zao na waathirika wakubwa ni watoto na wanawake.. wanaume wanakimbia familia zao,  hawana nafasi ya kukusanyika pamoja, “ alisema na kuongeza:

“Nawasihi watu wa Mungu pigeni magoti zaidi kuomba amani, yaombeeni pia mataifa mengine ili Mungu arudishe amani,” alisema.

Kuhusu chaguzi zitakazofanyika nchini mwaka huu, Bilal amewaomba Watanzania kujitokeza katika shughuli hizo muhimu ambazo zitawawezesha kuchagua viongozi wanaowataka waliongoze taifa.

“Rai yangu kwa viongozi wa dini zote liombeeni taifa letu ili shughuli hizi zifanyike kwa amani, Serikali imejipanga vizuri kusimamia shughuli hizi kwa ufanisi mkubwa,” alisema.

Pia aliwasihi waumini wa dini zote kuendelea kuvumiliana, kuheshimiana na kushirikiana.

Kuhusu maadili Bilal alisema amezitaka familia kuwafundisha vijana umuhimu wa kuheshimu kazi na siyo kushinda vijiweni.

Akizungumzia kuhusu sherehe hizo, Bilal alisema makanisa hayo yanamchango wa kimaendeleo katika nyanja tofauti ikiwemo elimu.

“Mnamiradi mingi ikiwa ni pamoja na kuanzisha shule ya watu wenye ulemavu wa ngozi,  mradi wa kusomesha watoto yatima na walio katika mazingira magumu iliyopo Kilimanjaro, Arusha na Tanga pamoja na mradi wa maji mjini Babati.”

Kuhusu changamoto za uhuru wa kuabudu kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Kisabato pamoja viwanja vya kujengea huduma za jamii na kanisa hasa maeneo ya mjini Bilal aliahidi kuyafanyia kazi.

Naye, Rais wa Wasabato Duniani, Askofu Ted Wilson, akizungumza na waumini wake alisema anaiombea nchi amani na mshikamano.

Sherehe hizo zimehusisha nchi 11 kutoka Afrika Mashariki na Kati ambazo ni Ethiopia, Uganda, Demokrasia ya Kongo, Burundi, Sudan Kusini, Elitria, Somalia, Jibuti, Uganda, Kenya  na Tanzania.
Kanisa la Wasabato kwa sasa linawaumini wasiopungua milioni 30.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!