Sunday, 25 January 2015
NIMEAIACHIA TANESCO MIRADI YA KUONDOA UMASKINI-MUHONGO
ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema pamoja na kujiuzulu, ameiachia Shirika la Umeme (Tanesco), miradi ya kuongeza uzalishaji umeme, ambao ni muhimu katika kuifanya nchi kuwa ya kipato cha kati miaka kumi ijayo.
Akizungumza jana Dar es Salaam kabla ya kujiuzulu, Muhongo alisema wakati baada ya Uhuru kulikuwa na mkakati wa kuunganisha Afrika kwa barabara kutoka Cape Town Afrika Kusini mpaka Cairo Misri, ameacha mradi kama huo wa kuunganisha Afrika kwa umeme.
Amefafanua kuwa kwa sasa Tanesco inanunua umeme kwa bei ghali ya senti za Marekani 30 mpaka 55, lakini kupitia mradi huo nchi za Afrika zitaweza kuuziana umeme, na Tanzania itaweza kununua umeme mpaka wa senti sita za Kimarekani kutoka nje na kuuza wa kwake.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, alipoteuliwa kushika nafasi hiyo Aprili 2012, alijua kuna dira ya taifa ya 2020-2025, yenye lengo la kuondoa umasikini nchini. Alisema kwa kuwa wizara hiyo ni nyeti katika utekelezaji wa dira ya maendeleo, aliamua kutekeleza mtazamo wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wa tangu mwaka 1969, ambapo alisema wakati nchi zilizoendelea zinakwenda mwezini, Tanzania waende vijijini.
“Kwa hiyo kazi yangu ya kwanza ilikuwa kwenda vijijini…niliongoza jahazi la Serikali kwenda vijijini kupeleka umeme,” alisema. Kutokana na kazi hiyo ya miaka miwili na nusu, Profesa Muhongo alisema sasa hivi vijiji 1,500 nchini, vinanufaika na umeme ambao gharama yake ya kuunganishwa ni Sh 27,000.
HABARI LEO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment