Jana Profesa Sosperter Muhongo alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini, akieleza kuwa anataka nchi isonge mbele kwa kuwa suala la kumtaka Rais amwondoe kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, limesababisha mambo mengi kukwama.
Profesa Muhongo amekuwa waziri wa pili kuondoka baada ya Profesa Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kuingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa IPTL, fedha ambazo zinahusishwa na sakata la escrow.
Mbali na mawaziri hao, tayari Jaji Fredrick Werema amejiuzulu kazi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa ushauri wake kuhusu fedha za escrow haukueleweka na kusababisha tafrani.
Pia, katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa sakata hilo, wakati watumishi watano wa Tanesco, Benki Kuu (BoT) na Mamlaka ya Mapato (TRA) wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kupokea rushwa inayohusu sakata hilo. Kashfa hii ni moja ya matukio mengi makubwa yaliyosababisha Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Baadhi ya matukio hayo ni kashfa ya Richmond, CAG na Operesheni Tokomeza ambazo zilisababisha Rais kupangua baraza lake.
Ni jambo la kupongeza kwamba angalau hatua zimechukuliwa kwa kiwango fulani katika kushughulikia tatizo hilo lililohusu uchotwaji wa takriban Sh306 bilioni kutoka kwenye akaunti hiyo iliyokuwa BoT.
Kitu cha ajabu ni hii tabia inayoendelea kujengeka ya kuibuka kwa kashfa, mawaziri kujiuzulu, kuundwa kwa baraza jipya na baadaye mambo kuendelea kama kawaida kusubiri kashfa nyingine kuibuka bila ya hatu za dhati kuchukuliwa kudhibiti matukio kama hayo.
Jambo la ajabu ni kwamba kila kashfa inapoibuka, hutumika nguvu nyingi kuizua au kutetea viongozi wa Serikali hadi mambo yanapoonekana kuwa yamekuwa makubwa ndipo hatua zichukuliwe.
Tumeona katika kashfa ya escrow zilitumika nguvu nyingi kutetea wahusika hadi maji yalipozidi unga ndipo hatua zilipochukuliwa na kushughulikia wahusika. Kitu kibaya ni kwamba hadi wakati hatua zinaanza kuchukuliwa, tayari Serikali inakuwa imeshafuka na wananchi wameshaumia.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri sasa yamekuwa ya kawaida kwa kuwa kila yanapofanyika hazichukuliwi hatua thabiti kuzuia kashfa zisitokee. Suala la fedha kuchotwa kwa fedha zinazokuwa BoT sasa linaonekana kuwa la kawaida kwa kuwa kashfa ya Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje lilipotokea, hakukuchukuliwa hatua madhubuti kuziba mianya kama hiyo kwenye taasisi hiyo nyeti ya fedha.
Tunadhani ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali kuweka misingi imara ya uongozi itakayowabana viongozi wetu kujiingiza kwenye kashfa kama hizo. Misingi hiyo pia ihusishe hatua kali ambazo zinaweza kuchukuliwa kwa viongozi ambao wataingia kwenye kashfa hizo kwa makusudi au uzembe ili kuzuia wengine kufanya mambo ya aibu na yanayoumiza wananchi.
Pia, siyo ufahari kuwawajibisha viongozi wakati ufisadi umeshafanyika kama ilivyokuwa kwenye sakata la EPA na sasa escrow kwa kuwa fedha za walipa kodi zinakuwa zimeshachotwa. Ufisadi unatakiwa uzuiwe mapema kuliepusha Taifa kupoteza mabilioni ya fedha na wanaowajibishwa wachukuliwe hatua kwa kujaribu kula njama za ufisadi na siyo kuadhibiwa kwa kufanya ufisadi.
Kadri Serikali inavyoonekana kuweka mikakati ya kuwakingia kifua watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ndivyo vitendo hivyo vinavyozidi. Serikali inatakiwa ionyeshe kuchukia ufisadi kwanza.
Na ikichukia ufisadi, basi kujiuzulu wa kuwavua madaraka wahusika kutakuwa ni moja ya hatua za kuwashughulikia wahusika wote nah ii itasaidia kupunguza vitendo hivyo.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment