Wazazi wa Miss Tanzania, Lilian Kamazima, Mzee Deus na mkewe Eva Kamazima (pichani kushoto) wameibuka na kueleza kuwa binti yao ni Mtanzania halisi.
Mzee Kamazima anayeishi Arusha aliibuka jana na kutoa tamko kuhusiana na tetesi zinazohusu utata wa uraia wa binti yake na kueleza kuwa Lilian ni mzawa halisi wa Tanzania na kupuuza uvumi unaoenezwa kuwa si Mtanzania.
Mzazi huyo alisema yeye ni balozi wa Mtaa wa Azimio, Elerai jijini Arusha na kwamba wameupokea ushindi wa binti yake kwa furaha kwa kuwa alistahili taji hilo siku ya fainali.
Juzi na jana, kwenye mitandao ya kijamii zilizagaa taarifa kwamba mrembo huyo siyo Mtanzania , bali raia wa Rwanda.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Kamazima ambaye alifuatana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwandago Investment Ltd, Faustine Mwandago ambayo ndiyo iliyomsimamia ushindi wake mkoani Arusha, mzazi huyo alipinga taarifa hizo kwa madai hazina chembe ya ukweli wowote.
Kamazima ,alisema kuwa binti yake alizaliwa Hospitali ya ya Mount Meru, Arusha miaka 18 iliyopita na kuanza elimu ya msingi katika Shule ya Burka.
Alisema kuwa alibatizwa katika Kanisa Katoliki, Burka na kwamba alimaliza elimu ya sekondari katika Shule ya Prime iliyopo Uzunguni jijini Arusha.
“Tuhuma hizo hazina ukweli wowote huo vyeti vyake vipo wazi, ni upuuzi tu nauita binti yangu alizaliwa hapa Arusha katika hospitali ya mkoa ya Mt Meru,”alisema Kamazima.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa yeye ni mzaliwa wa mkoani Kagera Kijiji cha Kishago Kanyansina na alibatizwa katika Kanisa Katoliki Kishogo na mama mzazi wa binti huyo ni mzaliwa wa Kilimanjaro.
Mama mzazi wa mrembo huyo, Eva Kamazima alisema kuwa wamefurahishwa na ushindi wa binti yao, kuvikwa taji la urembo huo huku akisisitiza kuwa hata hapo awali walifurahi mtoto wao kushika nafasi ya pili.
Alisema kuwa furaha ya ushindi waliyokuwa nayo katika ukumbi wa Mlimani City siku ya fainali ilikuwa ni ya juu kwa kuwa walifurahia mtoto wao kushika nafasi ya pili na waliridhika na matokeo kama kawaida
“Unajua sisi hata aliposhika nafasi ya pili tulifurahi lakini kwa kupewa hata hii ya kwanza tumefurahi pia,”alisema mama mzazi huyo ambaye pia ni mmiliki wa maduka ya Mwana Mwana Fashion ya jijini Arusha.
Aliwataka wakazi wa Arusha kumuunga mkono mtoto wao katika kusherehekea ushindi huo na kuvitaka vyombo vya habari hapa nchini kuthibitisha taarifa sahihi kuhusu mtoto wake kabla ya kuandika chochote.
Mkurugenzi wa Mwanadago Investment alisema kuwa wanajivunia kampuni yao kutoa mrembo wa taifa na kwa sasa wanajiandaa na maandalizi ya kumpokea.
No comments:
Post a Comment