Mwaka 1970 wakati wa hafla ya kusherehekea miaka 10 ya kuanzishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwalimu Julius Nyerere, alibainisha kazi kuu tatu za chuo kikuu.
Alisema mosi, ni kutoa taaluma ya juu itakayofanya kazi kama msingi wa utekelezaji au nguzo ya uchunguzi zaidi; pili, chuo kikuu ni kitovu cha kusafirisha taaluma hadi nje ya mipaka iliyozoeleka na tatu kuandaa nguvu kazi yenye uwezo wa hali ya juu inayohitajika katika jamii husika.
Miaka 44 baada ya hotuba hiyo ya Mwalimu Nyerere, utekelezaji wa kazi ya tatu kwa vyuo vikuu vingi nchini umezidi kulegalega na tafiti nyingi zinaonyesha kuwa vyuo hivyo vinazalisha nguvu kazi ‘isiyoiva’ kikamilifu na kuifanya ikose sifa katika soko la ajira.
Tofauti na mwaka 1960 wakati UDSM ikianza na wanafunzi 12 ambao waliipa heshima kubwa Tanzania kwa uweledi na umahiri, hivi sasa nchi ina wanafunzi wanaojiunga vyuo vikuu takriban 100,000 ambao waajiri wanasema wengi hawana sifa.Miezi michache iliyopita Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), lilitoa ripoti yake ya mwaka 2014 iliyobainisha kuwa nusu ya wahitimu wanaomaliza vyuo katika jumuiya hiyo, hawana sifa ya kuajirika kutokana kukosa ujuzi unaotakiwa katika soko la ajira.
Ripoti hiyo iliyotolewa na chombo hicho kilichoanzishwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kudhibiti ubora wa elimu wa vyuo vikuu, inabainisha kuwa Tanzania inashika nafasi ya pili kwa kuwa na asilimia 61 ya wahitimu wasioandaliwa vizuri. Uganda inaongoza kwa asilimia 63, Rwanda na Burundi asilimia 55 na Kenya asilimia 51.
Sababu za viwango duni
Ripoti hiyo inaongeza kuwa hatua za vyuo vikuu vingi kudahili wanafunzi wengi kuliko uwezo wao na ukosefu wa walimu, vimechochea kwa kiasi kikubwa kuzalisha wahitimu wasio na umahiri katika kazi.
Hata wahitimu wenyewe, baadhi wanakiri kuwa vyuoni hawakupata maarifa ya kutosha ya kutekeleza ipasavyo majukumu ya kazi iwe katika kuajiriwa au ajira binafsi.
“Mambo mengi ambayo hufundishwa hayatujengi kupambana na soko la ajira au kujiajiri,” anasema John Mbonaga, mhitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na kuongeza:
“Hata katika ujasiriamali, walimu wanatoa mifano na mafunzo ya watu waliofanikiwa bila kutuambia kinagaubaga watu hao walianzaje kufikia katika ngazi za juu.”
Anasema sababu kuu mbili zinachangia wahitimu kutokuwa mahiri: mosi, walimu wengi hufundisha kuajiriwa zaidi kuliko kujiajiri na pili, soko la ajira linahitaji watu wenye ufaulu mkubwa badala ya maarifa.
Idadi ya wahitimu wa elimu ya sekondari, vyuo na vyuo vikuu inazidi kuongezeka kila siku na takwimu za sasa zinakadiria kati ya vijana 600,000 hadi 800,000 kila mwaka wanaingia kwenye soko la ajira.
Wahitimu hao ni miongoni mwa asilimia 54 ya watu wasio na ajira wenye umri chini ya miaka 25 katika taifa la 10 duniani kwa kuwa na kundi kubwa la vijana. Hii ni kwa mujibu wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Restless Development yenye makao yake nchini Uingereza.
Ili kuondoka na utegemezi wa ajira na wanafunzi kutoiva kitaaluma, Mbonaga anashauri waajiri na vyuo wakae pamoja wajadili namna ya kuboresha mitalaa na kukubaliana njia bora za kutoa mafunzo kwa kuzingatia uweledi badala ya ufaulu.
“Mimi nafikiri kitendo cha waajiri kuhitaji mtu mwenye vyeti vyenye alama za juu, ndicho kinachoongeza wanafunzi wengi kuhangaikia mitihani badala ya kujifunza masuala ya ujasiriamali kwa umakini…Serikali itokomeze tabia hiyo,” anaeleza.
Suala la wahitimu kutoandaliwa kikamilifu lipo na linatishia ushindani wa Watanzania katika soko la ajira, kama anavyobainisha Meneja Mkuu wa kampuni ya kusambaza vyakula kupitia mitandao ya Hellofood.com, Sherrian Abdul.
Anasema Watanzania wengi hasa wahitimu wa vyuo vikuu, siyo wabunifu na hawajiandai kikamilifu wakati wa usaili ili kuwavutia waajiri.
Meneja huyo anasema inasikitisha kuona kundi kubwa la vijana takriban 300 waliokuwa wameomba kazi mbalimbali katika ofisi yake, walishindwa kujieleza na hata kutoa historia fupi ya kampuni wanayoombea kazi.
“Kama mtu anashindwa kujieleza mwenyewe, kutoa taarifa japo kwa ufupi juu ya kampuni anayoomba kazi, ambayo habari zake zipo mtandaoni kila mahali, hivi unategemea mwajiri gani atakubali kubeba hatari kama hiyo?” anahoji.
Anaongeza kuwa inashangaza kuona nchi yenye tatizo la ajira kama Tanzania, vijana wake waliosoma hawaonyeshi kuguswa pale wanapopigiwa simu na kuambiwa kuwa hawajafanikiwa kupata kazi.
“Vijana hawakuwa wamejiandaa kwa usaili na asilimia kubwa hawakuwa na vipaji na wanaoweza kufanya kazi kwa bidii,” anabainisha na kuongeza kuwa kila kampuni makini inataka wafanyakazi wazuri wenye vipaji.
Tatizo la wahitimu kutoandaliwa vizuri mara nyingi hubainishwa kuwa ni matokeo ya taasisi za elimu ya juu kutofanya vizuri kazi zao za kuwaanda vijana kupambana na maisha halisi pamoja na soko la ajira.
“Ukiletewa mazao mabovu uyaendeleze na matunda yake lazima nayo yatakuwa mabovu,” anasema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Tolly Mbwete na kuongeza;
“Kuna dhoruba katika mfumo mzima wa elimu na siyo tu vyuo vikuu… kwa bahati mbaya hata taasisi zetu za elimu ya juu nazo zimeshindwa kuboresha hali hiyo
Kuanzia ngazi za chini, Profesa Mbwete anasema watoto hawafundishwi vizuri kujieleza kwa Kiingereza na Kiswahili, pia hawaandaliwi kujenga hoja na ushupavu wa kufanya mambo bila woga.
Ili kukabiliana na hali hiyo, msomi huyo anasema inahitajika mikakati mikali ya kuwapa vijana mbinu za kujiajiri na kuwa weledi katika taaluma hasa kwa kuwapa mazoezi ya kuwashirikisha zaidi kuliko kuwasikiliza tu walimu kama ilivyo sasa katika vyuo vingi.
“Tunahitaji mageuzi makubwa kwa sababu tumeshindwa kuwawezesha vijana kuishi mitaani licha ya kufaulu mitihani. Tutumie Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kufundisha na kuboresha masomo ya ujuzi wa mawasiliano kama tunavyofanya chuoni kwetu,” anasema.
Mpango wa Serikali
Tatizo la wahitimu kutopikika kikamilifu linaitesa pia Serikali kiasi cha kuangalia njia mbadala za kulitatua, angalau vijana hao waweze kujisitiri kimaisha katika soko gumu la ajira nchini.
Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2014/15, Waziri Dk Kawambwa alisema moja ya masuala ya kuzingatia katika utungaji na utekelezaji wa sera za wizara yake kuboresha mfumo wa elimu ya juu.
“Katika mwaka huu wa fedha wizara itatekeleza mpango wa kuhuisha na kuoanisha programu za elimu ya juu pamoja na ufundi ili utoaji wa elimu hiyo uzingatie mahitaji ya soko la ajira kwa maendeleo ya taifa,” anasema.
Iwapo mpango huo wa Serikali utafanikiwa, vyuo vikuu vinaweza kuboresha utoaji wa elimu ya juu ikawa ya kujitegemea zaidi. Hata hivyo, wanafunzi wanahitajika kusoma kwa kusadifu mazingira ya soko la ajira kwa ama kujiandaa kujiajiri au kujifua zaidi ili waajiriwe.
CHANZO. MWANANCHI
No comments:
Post a Comment