Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa zinazotarajiwa kuanza kunyesha Oktoba mwaka huu, hasa ukanda wa Pwani na nyanda za juu Kaskazini Mashariki.
Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, mvua hizo zinaweza kusababisha mafuriko na magonjwa ya milipuko.
Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alisema jana kuwa utabiri huo umeonyesha maeneo mengi nchini yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani, hivyo kilimo kinapaswa kufanyika kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu. Alisema Mkoa wa Ruvuma utakuwa na mvua chache kwa hiyo wakulima lazima wapate ushauri kwa maofisa ugavi kujua mazao gani yalimwe.
Dk Kijazi alisema katika msimu wa vuli unaoanza Oktoba hadi Desemba, mvua hizo zitanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Morogoro, Unguja, Pemba, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Geita Simiyu, Shinyanga na Kigoma.
Pia alisema kunatarajiwa kuwa na joto la wastani upande wa Mashariki mwa Bahari ya Hindi.
Alisema mamlaka za miji zinatakiwa kuchukua hatua za kuhakikisha mifumo na njia za kupitisha maji zinafanya kazi ili kuepusha maji kutuama na kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu, kupoteza wa maisha na mali katika maeneo husika.
“Menejimenti ya maafa inatakiwa kuchukua hatua stahiki za utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa maji safi na salama na usambazaji wa dawa na chakula ili kukabiliana na majanga,”alisema.
No comments:
Post a Comment