Friday, 5 September 2014

MABASI YOTE CHAKAVU NCHINI YAKAMATWE!



GAZETI hili katika toleo lake la juzi, liliripoti juu ya operesheni maalumu inayoendelea kufanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).
Iliripotiwa katika habari hiyo kuwa tayari Sumatra imebaini mambo mengi katika mabasi mbalimbali, yanayofanya safari zake hapa nchini. Kwa mfano, imedhihirika kuwa mabasi mengi yanayokwenda mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, yamechakaa.



Mengi ni makuu kuu na bodi zake zimetoboka. Mabasi mengine rangi zake, zimepauka na yana matairi vipara baada ya kutumika muda mrefu.
Jambo lingine ambalo limegundulika katika mabasi hayo ni yamekuwa yakichanganya mbuzi, kuku na abiria kwa pamoja, vitu ambavyo ni kinyume na taratibu za kawaida za usafirishaji. Suala lingine lililobainika ni kuongeza ruti, ambazo hazikukatiwa leseni Sumatra.
Kwa mfano, baadhi ya mabasi ambayo yalitakiwa kutoa huduma kati ya Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam hadi Kimanzichana mkoani Pwani, kwa sasa yanafika hadi Kilwa Masoko wilayani Kilwa.
Makosa mengine ambayo Sumatra imeyabaini ni mawakala wa kampuni za mabasi, yanayosafirisha abiria kuongeza nauli. Kwa mfano, abiria wengi wanatozwa hadi Sh 28,000 kutoka Dar es Salaam hadi Mtwara badala ya Sh 24,000.
Tunaunga mkono hatua hizo ya Sumatra, kwa sababu zimelenga kuboresha huduma ya usafiri na kuondoa kero zote, zinazozorotesha sekta ya usafirishaji nchini.
Ni dhahiri mabasi yakiwa mabovu, huleta madhara mengi ya kiuchumi na kimaisha. Kwa mfano bodi la basi lililochakaa na lenye matundu, huingiza vumbi jingi ndani ya basi, hivyo kuathiri afya za abiria.
Basi kuu kuu lenye viti vilivyochakaa, huchana nguo za abiria na huwajeruhi mwilini kwa kukata ngozi zao. Pia, ni dhahiri mabasi mabovu, hupunguza idadi ya abiria wanaoyapanda, hivyo kupunguza mapato ya wamiliki wa mabasi hayo.
Ikumbukwe pia kuwa mabasi bora, huvuta watalii wengi, hivyo kulipatia Taifa fedha nyingi za kigeni. Aidha, tunapongeza Sumatra kwa kuzichukulia hatua kali kampuni za mabasi, yaliyozidisha nauli, ambapo tayari kampuni nne za mabasi yaendayo Lindi na Mtwara, zimepigwa faini ya Sh 250,000 kila moja.
Hatua kama hizi, zinatakiwa zisiwe za muda mfupi, bali ziwe endelevu na ziendeshwe katika mikoa yote nchini. Tunasihi Sumatra iendelee kukagua mabasi yote, yanayotoa huduma nchini, ikiwemo ya Lindi na Mtwara.
Ukaguzi huo ufanywe na wataalamu wa Sumatra kwa kushirikiana na Mkaguzi kutoka Jeshi la Polisi ili kuthibitisha iwapo mabasi hayo, bado yanakidhi viwango vya ufundi na usalama.
Pia, madereva wa mabasi, waendelee kujaribiwa na wataalamu wa Sumatra na Jeshi la Polisi kwa lengo la kujiridhisha, kama bado wana sifa za kuendelea kuendesha mabasi.
Aidha, tunapendekeza Sumatra ianze kuhamasisha wamiliki wa mabasi nchini, kununua mabasi ya kisasa na kuyapeleka mikoa ya Kusini, kwa sababu kwa sasa hakuna basi la daraja la Kwanza, linalokwenda katika mikoa hiyo

HABARI LEO.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!