Dodoma. Tukio la kutupwa kwa viungo vya binadamu jijini Dar es Salaam limewagusa baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba ambao sasa wamependekeza Katiba mpya itambue haki ya kuhifadhi maiti.
Viungo hivyo, ambavyo ni mikono, miguu vilivyokuwa katika mifuko 85 ya plastiki vikiwamo vichwa, miguu, mikono, mapafu, moyo, vifua na mifupa viliokotwa Julai mwaka huu eneo la Mbweni Mpiji jijini Dar es Salaam.
Mabaki ya viungo hivyo vya binadamu vilivyokuwa havitoi harufu, vilikuwa vikitumiwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba (IMTU) kwa ajili ya kufundishia.
Akiwasilisha maoni ya Kamati Namba Tisa juzi, mwenyekiti wa kamati hiyo, Kidawa Hamis Salehe, alisema kamati yake imependekeza wajibu wa kuhifadhi maiti uingizwe kwenye Katiba.
Kamati hiyo imependekeza Ibara ya 24 A (1) ya Katiba itamke kuwa kila mtu atakuwa na wajibu wa kulinda maiti dhidi ya udhalilishaji, kuikabidhi kwa jamaa au watu wanaostahiki.
Ibara ndogo ya pili inapendekeza kupigwa marufuku kwa mtu yeyote kufanya biashara ya kuuza au kusafirisha maiti au kiungo cha mwili wake kinyume na taratibu za nchi na mikataba ya kimataifa.
Mbali na ibara hiyo, ibara ndogo ya tatu imepinga Bunge kutunga sheria kwa ajili ya kulinda, kuhifadhi na kushughulikia maiti wakiwamo waliokosa jamaa zao katika maeneo ambayo mauti imewakumba.
“Hili tumeona, mfano wa vile viungo vilivyotupwa kwenye korongo na Chuo cha IMTU kwa hiyo tumepiga marufuku kufanya vitendo kama vile vya udhalilishaji,” alisema mwenyekiti huyo.
Pia kamati hiyo imependekeza kuongezwa kwa ibara ndogo ya 26 (2) ili kuzuia biashara haramu ya uuzaji wa viungo vya binadamu, ikiwamo viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi, yaani Albino.
“Kwa vile imebainishwa kuwa si binadamu peke yao ndio wanaouzwa katika Jamhuri ya Muungano bali hata viungo vya binadamu navyo vimekuwa vikiuzwa hasa kwa walemavu wa ngozi,” alisema Kidawa.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment