Thursday, 22 May 2014

KESI YA KUTOROSHWA KWA TWIGA KWENDA UARABUNI -MWANDISHI JELA BAADA YA MDHAMINI WAKE KUTOROKA

Mwandishi wa habari wa siku nyingi, Peter Temba amehukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kushindwa kumpeleka mahakamani mshtakiwa aliyemdhamini katika kesi ya kutorosha twiga kwenda Uarabuni.

Mwandishi huyo anayeandikia Gazeti la Serikali la Daily News na mwenzake aliyekuwa akiandikia Gazeti la Nipashe, Jackson Kimambo walimdhamini mtuhumiwa huyo raia wa Pakistan, Kamran Ahmed ambaye ni mshtakiwa namba moja katika kesi hiyo.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro ilitoa amri ya kuwakamata wadhamini hao baada ya mshtakiwa waliyemdhamini kwa kutia saini hati ya dhamana ya maneno ya (bond) ya Sh14.2 milioni, kutoroka.
Waandishi hao walimdhamini mshitakiwa huyo Juni 11, 2011 baada ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Moses Mzuna kuamuru kila mshtakiwa akabidhi mahakamani Sh14.2 milioni au mali yenye thamani hiyo.
Sharti la pili lilikuwa kila mshtakiwa katika kesi hiyo ya kutorosha twiga wanne na wanyama wengine 148 kwenda Uarabuni, kuwa na wadhamini wawili wakazi wa Kilimanjaro watakaosaini dhamana ya Sh14.2 milioni kila mmoja na waliojitokeza ni waandishi hao.
Kesi hiyo ikiwa katika hatua za usikilizwaji, Ahmed aliruka masharti ya dhamana na kwa miezi takriban mitano vyombo vya dola vimekuwa vikimtafuta kwa udi na uvumba bila mafanikio na hata wadhamini wake walishindwa kumpeleka mahakamani hadi ilipotolewa hati ya kuwakamata.
Temba alikamatwa Jumatatu wiki hii na kufikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi wa Mkoa Mfawidhi, Simon Kobelo na alipoulizwa alipo mshtakiwa huyo alisema hajui na hana Sh14.2 milioni alizosaini kama dhamana.
Wakili wa Serikali, Stella Majaliwa aliomba sheria ichukue mkondo wake kwa kuwa mshtakiwa katika kesi hiyo pamoja na mdhamini wa pili hawajulikani walipo.
Kobelo alisema sheria iko wazi na kwamba kulingana na Kifungu cha 160(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, mdhamini huyo atatumikia kifungo cha miezi sita jela.
Kufungwa kwa mwandishi huyo kumeibua simanzi kubwa miongoni mwa wanahabari na familia yake hasa ikizingatiwa kuwa ni mwaka jana tu, alikatwa mguu mmoja kutokana na maradhi ya kisukari
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!