Thursday, 22 May 2014

WANAFUNZI WASIO NA UWEZO KULIPIWA ADA

SERIKALI kupitia halmashauri zote nchini ina mpango wa kuwasaidia na kuwalipia ada na michango mingine wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo.


Kauli hiyoilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Kulthum Mchuhuli(CUF), aliyetaka kujua makakati wa serikali kuhusiana na wanafunzi ambao hawajapata matokeo yao kwa sababu ya kutolipa ada za mitihani.
“Siwezi sema wale wote asilimia saba ambao hawajalipa na kushindwa kupata matokeo yao kwamba ni masikini, lakini wanafunzi ambao hawalipiwi na halmashauri sisi wote na wahisani tunawajibu wa kuwasaidia ili waweze kupata matokeo yao,”alisema Waziri Kawambwa.
Katika swali la msingi, Mchuchuli alitaka kujua ni wanafunzi wangapi wa kidato cha nne ambao hawajapata matokeo yao kwa sababu ya kutolipa ada za mitihani.
Akiendelea kujibu swali hilo, Waziri Kawambwa alisema serikali itajitahidi kwa kila namna, ili wanafunzi hao wapate matokeo yao.
Alisema katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana, watahiniwa 31,518 kati ya watahiniwa 404,083 waliofanya mtihani huo matokeo yao yalizuiwa kwa sababu ya kutolipa ada.
Alieleza idadi hiyo ni sawa na asilimia 7.79 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo.
Hata hivyo, alisema matokeo yaliyozuiwa hufunguliwa mara moja baada ya mtahiniwa husika kulipa ada yake.
“Hadi Mei 8 mwaka huu, jumla ya watahiniwa 7,1314 wameshawasilisha ada zao na kufunguliwa matokeo yao na hivyo idadi ya watahiniwa ambao bado hawajawasilisha malipo yao ya ada ni 24,204,”alisema Dk. Kawambwa.
Aliwasihi wazazi na walezi wa watahiniwa ambao matokeo yao yamezuiliwa, kulipa ada hizo mapema, ili matokeo hayo yaweze kufunguliwa na kutoa fursa kwa wanafunzi hao kuendelea na kozi mbalimbali

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!