Saturday, 22 February 2014
UFAULU KIDATO CHA IV WAPANDA
UFAULU wa watahiniwa wa kidato cha nne mwaka jana umeongezeka kwa mujibu wa taarifa ya matokeo ya mitihani hiyo kutoka Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Katika matokeo hayo, wanafunzi 235,227 sawa na asilimia 58.25 ya watahiniwa wote wamefaulu, ikilinganishwa na yaliyotangazwa mwaka jana ambapo wanafunzi 185,940 sawa na asilimia 43.08 walifaulu.
Aidha, wanafunzi 10 wamefutiwa matokeo kwa kuandika matusi kwenye karatasi za majibu na 272 kwa kufanya udanganyifu.
Akitangaza matokeo hayo jana, Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk Charles Msonde alisema wasichana waliofaulu ni 106,792 sawa na asilimia 56.73 na wavulana ni 128,435 sawa na asilimia 59.58.
Alisema watahiniwa wa shule waliofaulu ni 201,152 sawa na asilimia 57.09 huku wasichana wakiwa 90,064 sawa na asilimia 55.49, wavulana ni 111,088 sawa na asilimia 58.45 wakati matokeo ya mwaka jana watahiniwa 159,747 sawa na asilimia 43.08 walifaulu.
Alisema watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu ni 34,075 sawa na asilimia 66.23 wakati mwaka jana walifaulu 26,193 sawa na asilimia 43.07 na watahiniwa wa mtihani wa Maarifa (QT) waliofaulu ni 6,529 sawa na asilimia 43.38 wakati mwaka jana walikuwa 5,984 sawa na asilimia 35.09.
Wasichana kiboko
Dk Msonde alisema katika matokeo hayo, wanafunzi 10 bora wasichana ni saba na wavulana ni watatu na kuwataja kuwa ni Robina Nicholaus, Sarafina Mariki, Janeth Urassa na Abby Sembuche wa sekondari ya wasichana ya Marian mkoani Pwani.
Wengine ni Magreth Kakoko na Angel Ngulumbi wa sekondari ya wasichana ya St. Francis, Mbeya na Joyceline Marealle wa sekondari ya Cannosa.
Wanaume watatu ni Sunday Mrutu wa sekondari ya Anne Marie, Dar es Salaam; Nelson Anthony na Emmanuel Gregory wa sekondari ya Kaizirege mkoani Kagera.
Dk Msonde alisema katika uchambuzi wa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja, watahiniwa wa shule 74,324 sawa na asilimia 21.09 wamefaulu katika madaraja ya kwanza hadi tatu wakiwamo wasichana 27,223 na wavulana 47,101.
Alisema daraja la kwanza waliofaulu ni 7,579, la pili 21,728, la tatu 45,017, la nne 126,828 na la sifuri ni 151,187.
Akizungumzia ufaulu wa kimasomo alisema umepanda katika masomo yote kwa asilimia kati ya 0.61 na 16.72 ikilinganishwa na mwaka jana, ambapo watahiniwa walifaulu zaidi katika somo la Kiswahili kwa asilimia 67.77 huku somo la Hesabu wakifaulu kwa kiwango cha chini cha asilimia 17.78.
Alisema viwango vya kupanga alama vilivyotumika ni A (75-100), B+(60-74), B(50-59), C(40-49),D(30- 39),E(20-29) na F(0-19) Shule bora Dk Msonde alizungumzia shule zilizofanya vizuri na vibaya kwa zenye watahiniwa 40 na zaidi kuwa ni Mtakatifu Francis ya Mbeya, ya Wavulana ya Marian ya Pwani, ya wasichana ya FEZA ya Dar es Salaam, Precious Blood ya Arusha na Cannosa ya Dar es Salaam.
Wengine ni ya Wasichana ya Marian, ya Wasichana Anwarite ya Kilimanjaro, ya Abbey ya Mtwara, ya Rosmini ya Tanga na Seminari ya Don Bosco, Iringa.
Alizitaja shule 10 za mwisho katika kundi hilo kuwa ni Kisima ya Pwani, Kitongani ya Kigoma, Tongani ya Tanga, Njechele, Kitonga na Mvuti za Dar es Salaam, Lumemo na Ungulu za Morogoro na Tambani na Nasibugani za Pwani.
Kumi bora Alitaja kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa pungufu ya 40 zenye jumla ya shule 1,099 kuwa ni Kaizirege ya Kagera, ya wasichana ya Alliance na Mwanza Alliance za Mwanza na Thomas More Machrina na Hellens za Dar es Salaam.
Nyingine ni Queens of Apostles- Ushirombo Geita, St. Joseph Kilocha Seminari ya Njombe, ya Wasichana ya Bethelsabs Iringa, Seminari ya St Mary’s Junior Pwani na Maua Seminari ya Kilimanjaro.
Pia alitaja shule 10 za mwisho katika kundi hilo kuwa ni Singisa na Uchindile za Morogoro, Hurui na Gwandi za Dodoma, Barabarani ya Ruvuma, Nandanga na Likawage za Lindi, Vihokilo ya Mtwara, Chongoleani ya Tanga na Rungwa ya Singida.
Dk Msonde alitaja wasichana 10 bora kitaifa kuwa ni Robina Nicholaus, Sarafina Mariki, Abby Sembuche, Janeth Urassa na Catherine Swai wa Marian.
Wengine ni Magreth Kakoko, Violet Mwasenga na Angela Ngulumbi wa St Francis Mbeya, Joyceline Marealle wa Canossa Dar es Salaam na Getrude Mande wa Precious ya Arusha.
Pia 10 bora kwa wavulana kitaifa ni Sunday Mrutu wa Anne Marie na Shabani Maatu wa Mivumoni Islamic Seminary za Dar es Salaam, Nelson Antony na Emmanuel Gregory wa Kaizirege.
Wengine ni Razack Hassan wa St. Mathew, Hamisi Msango wa EAGLES, Brian Laurent na Mohamed Ally wa Wavulana Marian zote za Pwani, Joshua Zumba wa UWATA Mbeya na Shahzill Msuya wa St Amedeus, Kilimanjaro.
Yaliyozuiwa
Akizungumzia matokeo yaliyozuiwa kuwa watahiniwa 31,518 wa shule ambao hawajalipa ada, matokeo yao yamezuiwa na yatatolewa watakapolipa huku 23 waliopata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mitihani kwa baadhi ya masomo watafanya mitihani mwaka huu kwa masomo yaliyoathirika.
“Wengine 24 waliopata matatizo hayo na kushindwa kufanya mitihani masomo yote nao wamepewa fursa kufanya mwaka huu,” alisema
Matusi
Akizungumzia waliofutiwa mitihani zaidi ya 10 waliobainika kuandika matusi, kuwa ni 272 waliofanya udanganyifu 242 ni wa shule, 19 wa kujitegemea na 11 wa Maarifa.
Alisema 61 walikamatwa na notisi ndani ya chumba, 171 kuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida, wanne kuingia na simu katika chumba cha mitihani, tisa kufanyiwa mitihani au kutumia majibu ya wengine.
Pia 13 kuwa na majibu tofauti na kubadilishana karatasi za majibu na 14 kukamatwa wakidhamiria kuiba mitihani.
“Hata hivyo, idadi ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu ni ndogo ikilinganishwa na mwaka jana waliokuwa 789,” alisema.
Mwaka huo, watahiniwa 427,679 waliandikisha kufanya mtihani wakiwamo wasichana 199,123 na wavulana 228,556 huku watahiniwa wa shule wakiwa 367,163 na wa kujitegemea 60,516.
Kati ya watahiniwa hao, 427,679 waliosajiliwa kufanya mtihani huo Novemba mwaka jana 404,083 walifanya na 23,596 hawakufanya.
Alisema watahiniwa wa shule waliofanya mtihani walikuwa 352,614, wa kujitegemea 51,469 na wa mtihani wa Maarifa 15,061.
HABARI LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment