Saturday, 22 February 2014

FIGO: MATATIZO YAKE NI TISHIO KWA MAISHA YA WATANZANIA


Gharama kubwa za matibabu zawakatisha matumaini.
Hapa duniani kuna maradhi aina nyingi yanayotisha, yakisumbua binadamu, kuwatia ulemavu hata kuwa chanzo cha uchumi kutetereka, wakati mwingine kusababisha kifo. Miongoni mwa maradhi hayo ni kuharibika kwa figo.

Ugonjwa huo unaelezewa kwamba siyo tu unaleta maumivu kwa mgonjwa, bali pia hautibiki kirahisi pamoja na gharama za matibabu husika kuwa kubwa na wengi kushindwa kuzimudu.
Wataalamu wa afya wanasema kuwa, zipo sababu kadhaa zinazosababisha maradhi katika figo kwa binadamu ikiwamo matumizi mabaya ya dawa hasa za maumivu, dawa za kienyeji, baadhi ya dawa za Kichina, uvutaji wa sigara na  unywaji wa pombe kupita kiasi.
Onesmo Kisanga, Daktari Bingwa wa Figo kutoka  Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH), Kitengo kinachoshughulika na tiba  ya usafishaji wa figo na damu(Renal Dialysis Unity) anasema kuwa tiba ya usafishaji wa figo  kwa kitaalamu (Dialysis), uhusika na utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu, pia sumu zitokanazo na vyakula au dawa.  Dk Kisanga anasema kuwa  tiba ya ‘Dialysis’ ni ya gharama kubwa kwa kuwa kila mgonjwa anapohitaji kuipata, hutakiwa kutoa kiasi Sh300, 000, huku akitakiwa kuipata tiba hiyo angalau mara tatu kwa wiki ambapo hugharimu Sh900,000.
“Hii huduma inafanyika hapa (MNH) katika Kitengo cha Renal Dialysis Unity,  na mgonjwa anatakiwa kuipata tiba hiyo  maisha yake yote,”anasema Dk Kisanga.
Anafafanua kuwa Dialysis ni mchakato wa kutoa maji yasiyohitaji kutoka kwenye damu ya mtu. Mchakato huo hufanyika baada ya figo kushindwa kufanya kazi na taka hizo kuingia kwenye mfumo wa damu. Kwa kawaida figo hufanya kazi ya kuchuja uchafu katika mwili, lakini baadhi ya watu huathirika na figo zao kushindwa kufanya kazi  ya kuchuja uchafu huo kutokana na sababu mbalimbali zilizoainisha awali.
Kwa mujibu wa Dk Kisanga, usafishaji wa figo hufanywa kwa wagonjwa ambao  figo zao zimeathirika kwa kiasi kikubwa na maradhi au hata kwa dharura.
Anafafanua kuwa mgonjwa hutundikiwa mipira maalumu, huku kwenye mashine kukiwa na figo ya bandia ambayo kazi yake ni kupitisha damu, kuisafisha na kuirudishwa mwilini.
Anaelezea kuwa kwenye mashine maalumu kunakuwa na mipira kadhaa ikiwamo ya kupitishia damu kupeleka kwenye figo bandia, inayofanya kazi kama ya mwilini na mirija mingine ambayo ni mikubwa kiasi inatumika kutoa maji yasiyohitajika mwilini na sumu, huku mingine ikitumika kurudisha damu safi mwilini.
“Mgonjwa hulala akifanyiwa tiba hii kwa saa nne, bila kuchomwa sindano ya usingizi, kwa kuwa haina maumivu makali. Vilevile mgonjwa hutobolewa eneo maalumu  mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira. Kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa,” anasema Dk Kisanga.

Anaongeza kuwa pamoja na tiba hiyo kuwa ghali, bado haina uhakika wa kupunguza tatizo kwa asilimia 100, bali kwa asilimia 40 hadi 50 pekee
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!