Kusaidia watu ambao kweli wanahitaji msaada ni suala la msingi sana kwani wanafarijika na kujiona nao wana watu wanaowajali.
Mwanamuziki maarufu nchini, Naseeb Abdul, ‘Diamond’, amesema anapenda kusaidia jamii kuliko kustarehe.
Diamond alisema katika mahojiano na gazeti hili kuwa anaposaidia jamii hukumbuka namna alivyowahi kusaidiwa, kwani katika maisha yake kabla ya kufikia mafanikio aliyonayo sasa, alisaidiwa sana na watu.
“Maumivu ya shida na uhitaji nayafahamu, ndiyo maana nikiitwa kwenye shughuli yoyote ya kijamii nafarijika sana, najikumbusha nilivyokuwa nahitaji msaada,” alisema Diamond.
Alisema hivi karibuni alikuwa Afrika Kusini kwenye mradi maalumu wa kupinga njaa Afrika, ambako pamoja na mambo mengine alikutana na wasanii wakubwa, alibadilishana nao mawazo na kupata kitu kipya kutoka kwao.
“Wakati mwingine ukifanya jambo moja linazaa lingine, ndiyo maana nasema ninaposaidia jamii kwa namna yoyote ile hufarijika kuliko ninapofanya starehe,” alisema Diamond.
Diamond alisema akiwa katika mradi huo nchini Afrika Kusini, alipata bahati ya kuzungumza na mkali wa muziki Afrika, Yvonne Chakachaka na kujifunza mengi kutoka kwake.
“Siku hazigandi, ipo siku nitakaa kwa muda na kuangalia tunaweza kufanya nini katika muziki na mwanamama huyu mwenye mengi ya kujifunza, nilikaa naye kwa muda mfupi, lakini nilichojifunza ni kama nimekaa naye mwaka mzima,”alisema Diamond
No comments:
Post a Comment