Friday, 31 January 2014

WANAJESHI WANNE MBARONI KWA MAUAJI MKOANI MBEYA

Wanajeshi wanne wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kikosi cha 44KJ, Mbalizi mkoani hapa wanaokabiliwa na kesi ya mauaji ya Petro Sanga, mkazi wa Mbalizi, juzi walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Mbeya Mjini na kusomewa maelezo ya mashahidi 13 pamoja na vielelezo sita dhidi yao.Mwanasheria wa Serikali Prosista Paul, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Omary Mwinchande (24), Rajabu Hassan (23), Richard Coastor (24) na Mussa Hassani.

Aidha mwanasheria huyo alidai mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 18,2012 saa 3:00 usiku eneo la DDC Mbalizi ambapo walimuua marehemu huyo (Sanga) kwa kutumia kisu.
Alidai kuwa washtakiwa walitekeleza mauaji hayo kwa madai ya kulipiza kisasi baada ya kudaiwa kuwa kuna mwanajeshi mwenzao aliyetajwa kwa jina la Godfrey Katete alishambuliwa kwa kupigwa na baadhi ya wananchi kwenye baa ya Power Pub eneo la DDC Mbalizi. Aidha, Paul alisema washtakiwa hao mara baada ya kufanya mauaji hayo pia walihamia katika baa nyingine na kuanza kuwapiga wananchi waliokuwapo katika eneo hilo.
Paul alisema katika shauri hilo, upande wa Jamhuri una mashahidi 13, ambao waliandika ushahidi wao pia, kuna ushahidi wa vielelezo sita vitakavyotumika katika kesi hiyo ikiwamo ripoti ya uchunguzi wa daktari aliyemfanyia uchunguzi marehemu huyo.
Alisema katika mashahidi hao, akiwamo Meneja wa baa ya Power Pub, Bosco Choga, pamoja na baadhi ya wahudumu katika baa hiyo, wengine ni maofisa wa JWTZ wa Kikosi cha 44Kj Mbalizi, na maofisa wa polisi. Hata hivyo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya, Gibert Ndeuruo, alisema mahakama yake haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, hivyo alipokea maelezo hayo na kuahidi kuyawasilisha Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye uwezo wa kusikiliza.
Alisema kwamba kesi ataipeleka Mahakama Kuu, ili iweze kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa, lakini washtakiwa hao wanayohaki ya kupata nakala ya maelezo ya kesi yao ili waweze kuyapitia

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!