MIAKA ya nyuma Tanzania ilionekana kama dampo la kuingiza bidhaa zisizo na ubora, hatua iliyosababisha baadhi ya wadau kulitupia jicho Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuliamsha.
TBS iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 3 ya mwaka 1975 na kuanza kazi Aprili 16, 1976; Sheria Na. 2 ya mwaka 2009 iliundwa baada ya ile ya kwanza kufutwa.
Kutokana na baadhi ya wadau wa shirika hilo kulalamika kuingizwa kwa nguo zisizo na ubora, TBS imeanza operesheni ya kutokomeza uingizaji, usambazajI na uuzaji wa chupi za mitumba.
Hatua hiyo imesaidia udhibiti wa bidhaa zinazoingizwa nchini hasa kutokana na shirika hilo kuwa na ushirikiano wa karibu na baadhi ya idara mbalimbali za serikali nchini.
Sheria mpya imelipa shirika hilo uwezo wa kusimamia shughuli za utayarishaji wa viwango na udhibiti wa ubora.
Pamoja na mikakati thabiti inayofanywa na shirika hilo kuhakikisha Watanzania wanapata bidhaa zilizo na ubora, hivi sasa TBS inaendeleza operesheni ya kupambana na uingizaji wa nguo za ndani.
Msemaji wa TBS, Rhoida Andusamile, anasema hatua hiyo ni utekelezaji wa matakwa ya agizo la sheria ya 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani zilizokwisha kutumika.
Licha ya unafuu wa gharama za upatikanaji wa nguo za mitumba nchini, shirika hilo litaendelea kusimamia sheria na kupambana na wauzaji holela wa nguo hizo zikiwemo soksi, nguo za kulalia, sidiria na chupi.
Uelewa wa wananchi
Bado kuna tatizo kubwa hasa la kielimu katika kutekeleza operesheni hiyo, hii inatokana na ukweli kuwa nguo hizo zimekuwa zikiwasaidia watu wengi hasa wale walio na kipato cha chini.
Utafiti unaonyesha kuwa nguo za ndani mpya zimekuwa zikiuzwa kwa bei ya juu kwa kuanzia sh 5,000 na kuendelea, soksi zinauzwa kwa sh 1,000 na kuendelea. Nguo za kulalia zinaanzia sh 7,000 hadi 10,000, inategemea na aina yake.
Hivyo kutokana na gharama hizo kuwa juu wengi wa kipato cha chini na wale wa cha kati wamekuwa wakikimbilia kununua nguo za mitumba zinazouzwa kuanzia sh 300 hadi 5000.
Kutokana na hali hiyo nguo hizo zimeonekana kuwa na unafuu zaidi ingawa wataalamu wengi wamekuwa wakisema kuwa zina madhara kama zitakuwa hazijafuliwa na kupigwa pasi vizuri.
Wapo wanaosema kuwa kuna haja ya kutoa elimu ya ufahamu zaidi juu ya madhara yanayoweza kuwapata watu kuhusiana na matumizi ya nguo hizo.
Pamoja na kuanza kwa operesheni hiyo bado TBS wanapaswa kuwa na mkakati thabiti wa kutokomeza uuzaji wa nguo hizo kutokana na masoko yake kuendelea kuwepo.
Changamoto TBS
Andusamile anasema nguo za ndani za mitumba zinazouzwa hivi sasa katika masoko mbalimbali nchini zimeingia kupitia njia za panya (haramu) ambapo anawataka wauzaji wadogo kusaidiana na TBS kuwataja wakala wakubwa.
Anasema TBS imefanikiwa kudhibiti uingizwaji wa nguo hizo katika bandari, mipaka na viwanja vya ndege ingawa hadi sasa bado nguo hizo zinaonekana kuuzwa katika masoko.
Anasema kuwa operesheni hiyo haikuanzishwa kwa ajili ya kuwaumiza wafanyabiashara wadogo bali ni kutaka kuwaelimisha juu ya athari za kuuza nguo hizo na kutotakiwa kuwepo katika masoko ya hapa nchini.
Ofisa huyo anasema wanapofanya msako na kuwakamata wauzaji hao wanahakikisha nguo hizo zinachomwa moto na muuzaji kulazimika kulipa sh 50,000,000.
Kutokana na hatua hiyo ni ishara kuwa shirika hilo limekusudia kuwalinda Watanzania ili kuwaepusha na maradhi yatokanayo na matumizi ya nguo hizo kwa vile nguo hizo hazina ubora na hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Ipo haja kwa Watanzania kuhakikisha inaunga mkono jitihada hizo ili kupunguza madhara yanayoweza kupatikana kutokana na matumizi ya nguo hizo.
Mtaalamu wa ngozi azungumza
Daktari wa magonjwa ya ngozi, Anngie Krogh anasema kuna madhara makubwa yanaweza kuwapata watumiaji wa nguo hizo hasa kutokana na maeneo hayo yanayovaliwa kuwa na unyevu nyevu mara zote.
“Pamoja na kutakiwa kufuliwa, kuanikwa juani na hata kupiga pasi, bado nguo hizo zinahitaji zifuliwe kwa kutumia sabuni ya dawa yoyote ya kuua vijidudu, yapo magonjwa mengi ya ngozi ya kuambukizwa ndiyo maana mara zote tuna shauri kuepuka kuvaliana nguo,” anasema.
Anasema zipo takwimu zinaonyesha kuwa wanawake wengi ndio wanaofika katika hospitali za magonjwa ya ngozi kuhitaji huduma za matibabu na hiyo inasababishwa na maumbile ya wanawake ambayo ni rahisi kuambukizwa tofauti na wanaume.
Anatolea mfano vijidudu vya fangasi vimekuwa vikiwaathiri zaidi kina mama na kama wasipopata tiba mapema kuna uwezekano wa kuathiriwa zaidi katika mifumo ya uzazi.
TBS pekee haiwezi kufanikisha suala hilo ingawa wanashirikiana na vyombo vya dola lakini kubwa linalohitajika ni kuwepo kwa ushirikiano na Watanzania hasa wafanyabiashara wa nguo hizo.
Hilo likifanyika na wananchi wakielewe madhara yake operesheni ya kutokomeza nguo za ndani za mitumba itafanikiwa
TANZANIA DAIMA.
No comments:
Post a Comment