Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospiter Muhongo, amejigamba kuwa Tanzania haitadanganyika tena kwa wawekezaji wa sekta ya madini kutolipa kodi na kuifanya nchi kutofaidika na rasilimali zake.
Alisema hayo juzi katika mahojiano na waandishi wa habari baada ya Serikali za Tanzania na Finland, kutiliana saini, makubaliano katika kutafiti na kukuza sekta ya madini.
“Kama ni kutuibia walifanya hivyo siku za nyuma, lakini kwa sasa hawawezi tena,” alijigamba Profesa Muhongo akidai historia inaonyesha kuwa nchi zote zenye rasilimali za madini, mwanzoni zilidanganyika.
Alikiri kuwa awali wawekezaji katika migodi walikuwa wakijitetea kuwa walikuwa wanapata hasara lakini kwa sasa, sheria inawalazimisha kulipa asilimia 30.
Kauli ya Profesa Muhongo ilitokana na waandishi kumbana, kuhusu Watanzania kutonufaika na sekta ya madini wakati ina faida kubwa.
Profesa Muhongo alisema kwa sasa sekta ya madini inachangia asilimia 3.5 ya pato la Taifa.
Alisema malengo ni kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia zaidi ya asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Mapema, wakurugenzi wa sekta ya madini katika Serikali za Tanzania na Finland, walitiliana saini ya kukuza na kuendeleza sekta ya madini hapa nchini.
Akizungumzia makubaliano hayo, Profesa Muhongo alisema yanazingatia mambo matatu, ambayo ni pamoja na utafiti wa madini katika mikoa ya kusini.
Alisema kimsingi tayari wamegundua kuwa ukanda huo una makaa ya mawe, shaba, niko na platiniamu.
Alisema watakachokifanya ni kuainisha maeneo yenye madini na viwango halisi ili wakipatikana wawekezaji wa kuyachimba, waingie kwenye makubaliano ya uhakika.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment