Rais Magufuli alifariki dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena mkoani Dar es Salaam. Magufuli alikuwa Rais wa Tanzania kwa miaka mitano na miezi minne tangu Novemba mwaka 2015.
Machi 17 mwaka huu saa 5.03 usiku Rais Samia Suluhu Hassan wakati huo akiwa Makamu wa Rais, alitangaza kifo cha Rais Magufuli na zikatangazwa siku 21 za maombolezo na bendera kupepea nusu mlingoti nchi nzima.
Kwa mujibu wa takwimu, leo ni siku ya 21 tangu kutangazwa kwa siku hizo za maombolezo.
Wananchi katika maeneo ya Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na Geita walipata fursa ya kutoa heshima za mwisho kumuaga Rais Magufuli.
Nchi kadhaa za Afrika ziliungana na Tanzania kutangaza maombolezo na kushushwa bendera nusu mlingoti kwa siku kadhaa zikiwemo Msumbiji, Botswana, Comoro, Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda.
Viongozi kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo marais 10 walihudhuria mazishi kitaifa kwenye Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma Machi 22, mwaka huu.
Marais hao ni Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Filipe Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Felix Tshisekedi.
Wengine ni Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, Rais wa Botswana Mokgweetsi Masisi, Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani, Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, Rais wa Zambia Edgar Lungu na Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anapofariki dunia, nafasi yake hushikwa na aliyekuwa makamu wa rais hadi kipindi cha uchaguzi kinapowadia.
Kutokana na Katiba hiyo, baada ya kifo cha Rais Magufuli Machi 17, 2021, Samia Suluhu aliyekuwa Makamu wa Rais aliapishwa Machi 19, mwaka huu kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi kipindi cha uchaguzi kitakapofika mwaka 2025.
Rais Magufuli alizikwa Machi 26 mwaka huu nyumbani kwake Chato mkoani Geita.
No comments:
Post a Comment