WATANZANIA 40,000 watanufaika kwa kupata ajira kwenye mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Ajira 10,000 kati ya 40,000 zitakuwa za moja kwa moja na zilizobaki 30,000 zitatokana na watoa huduma mbalimbali wakiwemo mama ntilie au mama lishe. Mradi huo ambao utazinduliwa Jumamosi ijayo na Rais John Magufuli na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, utagharimu Sh trilioni nane (Dola za Marekani bilioni 3.5) na utakamilika mwaka 2020.
Ili kuhakikisha kuwa fedha hizo Sh trilioni nane zinawanufaisha zaidi Watanzania, Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) imepewa jukumu na serikali kuhakikisha kuwa inawaunganisha Watanzania wote wanaotaka kuwekeza kwenye fursa mbalimbali zitakazoletwa na mradi huo wa bomba.
Mmoja wa waanzilishi ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa ATOGS, Abdulsamad Abdulrahim alisema kwa muda mrefu Watanzania wamekuwa wakibaki nyuma kwenye miradi mbalimbali inayowekezwa nchini.
Abdulsamad alisema kwamba lengo la ATOGS ni kuwaunganisha watoa huduma mbalimbali kutoka sekta binafsi nchini kuchangamkia fursa za kibiashara kama vile usafirishaji, uhandisi, ujenzi, bima, ulinzi, chakula, huduma za kifedha za kibenki, vifaa vya ujenzi, huduma za kisheria na mawasiliano kwenye mradi huo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Dk Juliana Pallangyo alisema Watanzania waache kulalamika na badala yake waungane na ATOGS kuchangamkia fursa za kibiashara, na kutoa mwito kwa wananchi wa Tanga na mikoa jirani kujitokeza kwa keshokutwa ambako Rais Magufuli na Rais Museveni wataweka jiwe la msingi.
Kwa upande wao, Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) walisema asilimia 80 ya ujenzi wa bomba hilo utafanyika Tanzania na litapita kwenye mikoa nane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Singida, Tabora, Dodoma, Manyara na Tanga.
No comments:
Post a Comment