Wednesday 20 July 2016

Wanachuo 382 sasa warejeshwa UDOM

WANACHUO 382 kati ya 7,805 waliokuwa wanasoma Stashahada Maalumu ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wamerudishwa chuoni baada ya kukidhi vigezo vinavyotakiwa.


Aidha wanafunzi wengine 52 waliopata daraja la nne kinyume na matakwa ya programu hiyo hawataendelea na masomo kwa kuwa hawana sifa hiyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema hayo Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wanafunzi hao ambao walirejeshwa nyumbani na serikali Mei 28, mwaka huu. Profesa Ndalichako alisema baada ya hatua ya kuwaondoa wanafunzi hao chuoni kuchukuliwa, serikali ilifanya uchambuzi kwa lengo la kujiridhisha na sifa zao.
Alisema sifa zilizotakiwa ni ufaulu wa daraja la kwanza hadi la tatu na alama mbili au zaidi za ufaulu katika masomo ya Sayansi na Hisabati. Alisema wanafunzi hao waliorudishwa UDOM wana ufaulu wa daraja la kwanza hadi la pili, ambao pia wamefaulu masomo mawili ya sayansi kwa kiwango cha C – A.
“Wanafunzi hao 382, wa mwaka wa kwanza ni 134 na wa mwaka wa pili ni 248. Hao ndio pekee watakaorudishwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma ili wakamalizie mafunzo yao katika chuo hicho,” alisema.
Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wengine 4,586 wa mwaka wa kwanza wa programu hiyo maalumu ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu, watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo yao.
Vile vile wanafunzi 1,337 wa mwaka wa pili, watahamishiwa kwenye vyuo vya ualimu vya Korogwe na Kasulu kumalizia masomo yao.
“Wanafunzi 290 waliokuwa wamedahiliwa kusoma programu maalumu ya Stashahada ya Ualimu wa Elimu ya Sekondari masomo ya Sayansi na Hisabati ambao hawana sifa stahiki wanashauriwa kuomba mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo kwenye chuo chochote wanachotaka wao,” alisema Waziri huyo.
Ndalichako alisema wanafunzi waliokuwa wanasoma Programu ya Ualimu wa Elimu ya Msingi, hawakuwa sehemu ya programu maalumu ya kupunguza uhaba wa walimu wa sekondari wa Sayansi na Hisabati, ila walikuwa wanaandaliwa kufundisha shule za msingi tofauti na lengo maalumu la kukabiliana na uhaba wa walimu wa sekondari.
Alisema hata maudhui waliyokuwa wanasoma hayakuwa sawa sawa na yale ya Programu ya Ualimu wa Sekondari wa Sayansi na Hisabati. Waziri alisema wanafunzi 29 wa mwaka wa pili wenye cheti cha daraja la tatu A, waliodahiliwa kusoma Stashahada ya Ualimu wa Shule za Msingi, watahamishiwa katika Chuo cha Ualimu Kasulu wamalizie masomo yao kwa gharama zao wenyewe.
Pia wanafunzi 1,181 waliodahiliwa kusoma Stashahada ya kawaida ya Ualimu wa Elimu ya Msingi, waombe mafunzo yanayolingana na sifa walizonazo mahali popote watakapotaka wao. Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaorejeshwa UDOM.
Pia kwa wale watakaohamishiwa kwenye vyuo vya ualimu vya serikali, watapewa mkopo wa kiasi cha Sh 600,000 kwa mwaka ambayo ni ada ya mafunzo ya ualimu itakayolipwa moja kwa moja chuoni.
Alisema wanafunzi wote wanaorejeshwa UDOM, wataanza masomo Oktoba mwaka huu na wale wanaohamia vyuo vingine vya ualimu, wataendelea na mafunzo yao Septemba, mwaka huu.
Pia wanatakiwa kuripoti wakiwa na vyeti vyao halisi vya kidato cha nne ambavyo vitahakikiwa kabla hawajapokelewa rasmi kwenye vyuo walivyopangiwa. Alisema majina ya wanafunzi wenye sifa na vyuo walivyopangiwa pamoja na wale wasio na sifa, yanapatikana katika tovuti ya Wizara pamoja na tovuti ya Chuo Kikuu cha Dodoma.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!