Wednesday, 20 July 2016

MAHAKAMA YA TANZANIA YAKUSUDIA KUBADILISHA MUONEKANO WAKE

mahakama-kuu






Na Lydia Churi- Mahakama ya Tanzania
…………………………………………
Mahakama ya Tanzania imeamua kuchukua juhudi za makusudi ili kubadilisha muonekano wake na kuwa chombo kitakachojibu maswali na kuondoa kiu ya watanzania katika kupata haki kwa wakati.


Akifungua Mkutano wa Mahakama ya Tanzania na wadau wake wa kujadili utekelezaji wa Mpango Mkakati wa mhimili huo leo mjini Dodoma, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya Dodoma Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko amesema Mahakama ya Tanzania inakusudia  kukibadilisha chombo hicho ili kiweze kutoa haki kwa wakati kwa mujibu wa jukumu ililopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema katika kufanikisha azma hiyo, Mahakama ya Tanzania inaendelea na mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi wake yanayolenga kuuboresha Mpango Mkakati wake kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na taswira ya mahakama inakuwa chanya wakati wote.
Jaji Kwariko amesema Mahakama imeamua kuwashirikisha wadau kwenye Mpango Mkakati wake kwa kuwa umuhimu na nguvu waliyonayo Sitasaidia kufanikisha utendaji wa Mahakama katika kuyafikia malengo ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, Jaji Kwariko aliwataka watumishi wa Mahakama ya Tanzania kufanya kazi kwa bidii katika kuutekeleza Mpango Mkakati kwa kuwa utendaji kazi wao utapimwa kwa jinsi watakavyotekeleza majukumu yao kulingana na Mpango Mkakati huo. Aliongeza kuwa Mahakama ya Tanzania itaelekeza rasilimali zake zote kama vile watu, fedha na muda katika kuleta matokeo makubwa yanayotarajiwa.
Alisema endapo watumishi hao watajikita katika kufanikisha uimara wa nguzo zote tatu za Mpango Mkakati huo,  upatikanaji wa haki kwa wakati na uhusishwaji wa wadau na imani ya wananchi vitakifanya chombo hicho kutimiza ndoto yake na kuifikia dira yake. Nguzo tatu za Mpango Mkakati huo ni Utawala bora, Uwajibikaji na Usimamizi wa rasilimali.
Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mheshimiwa Katarina Revokati alisema baada ya Mpango Mkakati wa Mahakama kukamilika, watumishi watasaini kadi itakayokuwa ikionyesha namna ya utekelezaji wa Mpango Mkakati na kadi hiyo itaweka alama za kuonyesha ufaulu katika utekelezaji, endapo mtumishi atapata alama ndogo atachukuliwa hatua.
Akizungumzia namna Mahakama inavyopambana na rushwa, Msajili huyo alisema Mahakama imeweka mazingira ya uwazi katika utoaji wa huduma zake pamoja na kuweka mifumo ya kielekitroniki na kuhusisha wadau wake katika utendaji kazi wake.
Mahakama ya Tanzania inaendelea na Mafunzo ya wiki mbili kwa watumishi wake kuhusu uandaaji na utekelezaji wa Mpango Mkakati wake ambapo leo ilikutana na wadau wake ili kujadili namna ya utekelezaji wa Mpango huo.
Wadau waliohudhuria, mafunzo hayo leo ni Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Polisi Makao Makuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-TAKUKURU na Wakala wa Majengo Tanzania-TBA.
Wengine ni pamoja na Baraza la Habari Tanzania-MCT, Tume ya Kurekebisha Sheria, Tume ya Usuluhishi wa Migogoro, Ofisi ya Nyaraka za Taifa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!