Thursday 21 July 2016

Mtoto aliyewekewa kifaa kwenye moyo aruhusiwa

Mtoto Happiness John (6) aliyefanyiwa upasuaji
Dar es Salaam. “Natamani kurudi Arusha niende shuleni, nataka kuwa daktari.”
Ndivyo alivyosema jana mtoto Happiness John, mkazi wa Seliani Arusha baada ya kuhakikishiwa ruhusa ya kuondoka hospitalini kutokana na hali yake ya kiafya kuendelea kuimarika.


Happiness ambaye alifanyiwa upasuaji kwenye moyo na kupandikiziwa kifaa cha kusaidia kudhibiti mapigo ya moyo (Pacemaker) Julai 15, alikuwa akisoma shule ya chekechea ya Hilltech iliyopo mjini Arusha.
Elitruda Malley ambaye ni mama wa Happiness, alisema binti yake mwenye umri wa miaka sita alishindwa kusonga mbele kielimu kutokana na kuzirai mara kwa mara, kulikosababishwa na tatizo la moyo.
Alisema mtoto wake kwa sasa anaendelea vizuri na amekuwa mchangamfu ikilinganishwa na kipindi cha nyuma kabla ya kufanyiwa upasuaji.
Akizungumzia afya ya Happiness, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Prof Mohamed Janabi alisema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri na leo wanatarajia kumruhusu baada ya kukamilisha sindano moja aliyotakiwa kuchomwa jana jioni.
Alisema kutokana na utabibu aliofanyiwa binti huyo, kifaa hicho kitalazimika kubadilishwa betri baada ya miaka 10, lakini kutokana na utafiti mpya ulioanza kufanywa nchini Marekani huenda betri aliyonayo ikachajiwa nje pasipo kufungua kifua cha Happiness kwa mara nyingine.
Alisema mpaka sasa JKCI imefanikiwa kufanya upasuaji wa aina hiyo kwa watu 15 wenye umri mkubwa tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Hii ni mara ya kwanza kwa JKCI kufanya upasuaji huo kwa mtoto.
Msemaji wa JKCI, Mohamed Maulid alisema kabla ya kufanyiwa upasuaji huo, mtoto huyo alikuwa akipata shida kupumua kutokana na mapigo ya moyo kushuka mpaka kufikia 20 na sasa yamekuwa yakipanda kwa kiwango cha 60-80.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!