Thursday 21 July 2016

Vyeti walohitimu vyuo vikuu kijanja kufutwa




Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati akifungua Maonesho ya 11 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia.


SERIKALI itahakiki na kufuta vyeti vya wahitimu wa vyuo vikuu nchini, ambao walijiunga na masomo ya elimu ya juu bila ya kuwa na sifa.Aidha, serikali imetangaza pia kuhakiki na kisha kufuta udahili wa wanafunzi walio vyuo vikuu ambao pia wamejiunga na masomo ya elimu ya juu bila ya kuwa na sifa.



Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukagua maonyesho ya 11 ya vyuo vikuu jana, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alisema msako kukagua wanafunzi walioingia vyuoni kwa hila utaanza wakati wowote baada ya kumalizika kwa ukaguzi wa wanafunzi hewa waliopata mikopo.
Maonyesho ya vyuo vikuu yanaratibiwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na yalifunguliwa na Waziri Ndalichako jijini Dar es Salaam jana.
Juzi serikali ilifuta udahili wa wanafunzi 7,423 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waliokuwa wakisoma stashahada ya ualimu wa sekondari na msingi ya masomo ya Sayansi na Hisabati, baada ya kubaini waliingia bila kuwa na sifa.
Prof. Ndalichako alisema msako huo kabambe unaokuja dhidi ya wanafunzi wasio na sifa utahusisha wale wa kuanzia mwaka wa kwanza mpaka walipo makazini, waliomaliza miaka ya nyuma, ili mradi wawe walifanya udanganyifu.
“Labda nikwambie tu kwamba sifa zote za wanafunzi walioko vyuo vikuu ninazo kwenye komputa yangu," alisema Prof. Ndalichako. "Hata hapa kwenye 'ipad' (yagu) nikikuonyesha, wote sifa zao ninazo."
"Na wanafunzi wote walioingia vyuo vikuu sifa zao sasa hivi zinafanyiwa uhakiki, na ni kwa mwanafunzi yeyote yule haijalishi ni wa mwaka wa kwanza wa pili au wa tatu.
"Kama aliingia hana sifa tutamnyofoa tu, na hata kama amemaliza lakini alipita chuoni kwa udanganyifu na yuko kazini naye tutamnyofoa tu.”
Aidha, Prof. Ndalichako alisema kazi ya kuhakiki wanafunzi wasio na sifa ilitakiwa ianze kabla ya kuhakiki wanafunzi hewa, lakini waliamua kwanza kulimaliza hilo.
“Hilo suala la kuhakiki wanafunzi wasio na sifa ni endelevu kwa sababu kuna watu ambao wamekuwa wakiingia vyuoni kwa njia wanazozijua wenyewe.
Na tutakuja kuangalia nani aliyekuwa anahusika na kufanikisha hilo. "Lakini kama kuna watu wanafahamu waliingia kwa ujanja ujanja, wasipoteze muda wao na rasilimali zao kuendelea kujigharimia wakati wanajua wameingia na sifa zisizo sahihi, maana tunaenda kuwanyofoa.
” Wakati akitangaza kufukuzwa kwa wanafunzi 7,423 wa UDOM juzi, Prof. Ndalichako alisema wanafunzi wengine 52 walikuwa wamepata daraja la nne na hivyo kukosa sifa za kusoma stashahada.
Wanafunzi wengine, Prof. Ndalichako alisema, serikali itawapangia vyuo vingine vya ualimu kuendelea na masomo mengine, lakini siyo kozi hiyo maalumu ambayo ililenga kupunguza uhaba wa walimu wa sayansi na hisabati.
Alisema wanafunzi 290 walibainika kukosa vigezo vingine ikiwa ni pamoja na kufeli masomo ya sayansi, hivyo wametakiwa kujiunga na taaluma nyingine kulingana na sifa walizonazo, Prof. Ndalichako alisema.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Kaimu Katibu Mtendaji wa TCU, Eliuta Mwageni alisema lengo la tume hiyo ni kuhakikisha wanafunzi wanaoingia kwenye vyuo hivyo wanakuwa na sifa stahiki.
Kuhusu wanafunzi waliofukuzwa Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), kutoka na kubainika kuingia chuoni hapo bila sifa, alisema kilichotokea ilikuwa ni udhaifu wa utendaji na kwamba kiutaratibu halikupaswa kutokea.
“Utaratibu ambao tunatumia kudahili wanafunzi wa vyuo tunashirikiana na Baraza la Mitihani (Nacte), ambao huwa wanatupatia namba ya mwanafunzi akimaliza kidato cha nne, ambayo ndiyo kitambulisho tosha kinachotuonyesha kwamba alikuwa na sifa za kumpeleka kidato cha sita, na kwa sifa zile ndipo anaweza kuingia chuo kikuu," alisema Mwageni.
"Mfumo wetu ulivyo kama huna sifa huwezi kuingia.” Alisema waliohusika katika kudahili wanafunzi wa Udom ambao hawakuwa na sifa watachukuliwa hatua kali.
"Tunachoomba ni kwamba wanafunzi ambao hawana sifa wasidanganyike, ukitumia gharama nyingi huna sifa utaondolewa tu.”

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!