Wednesday, 18 May 2016

Waliorekodi video ya kujamiiana kortini leo

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei.

VIJANA wawili wanaoshikiliwa na Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za kumbaka msichana, kumpiga picha za utupu za video na kuzisambaza katika mitandao ya kijamii, wametajwa kuwa waliweka makazi katika eneo la Dakawa wilayani Mvomero kwa takribani mwezi kabla ya kufanya kitendo hicho.


Watuhumiwa hao wanaotarajiwa kufikishwa mahakamani leo sanjari na wengi tisa waliosambaza video hiyo, imeelezwa kuwa walifikia kwenye nyumba ya kulala wageni ya Titii iliyopo kata ya Dakawa na waliishi kwa muda huo wakijishughulisha na kilimo.

Zuberi Thabiti (30) mkazi wa Mbarali, mkoani Mbeya pamoja Iddy Adamu (32) mkazi wa Makambako wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka msichana mwenye umri wa miaka 21, tukio linalodaiwa kufanyika Aprili 28 mwaka huu.

Baadhi ya ndugu wa watuhumiwa tisa wa kusambaza picha za utupu za msichana huyo , waliliambia gazeti hili kuwa kati ya hao, sita ni ndugu wa familia moja. Awali, akitoa taarifa jana mjini hapa kwa waandishi wa habari juu ya tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema uchunguzi na taratibu nyingine zilikuwa zinakamilishwa kwa ajili ya kufikisha watuhumiwa hao mahakamani leo.

Kamanda Matei alisema msichana huyo aliitwa na Zuberi anayesadikiwa alikuwa na uhusiano naye kimapenzi ; kwa minajili ya kuangana naye kwa vile alikuwa akitarajia kurudi kwao Mbarali, mkoani Mbeya .

Alisema kuwa baada ya kuingia chumbani muda mfupi mlango wa chumba hicho uligongwa kwa nje na Zuberi alikwenda kufungua mlango ndipo alipomwona Iddy ambaye aliingia ndani akiwa ameshikilia kisu mkononi na simu.

Kwa mujibu wa kamanda, kabla ya tukio hilo, inadaiwa msichana huyo kabla ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na Zuberi , alishawahi kuwa na mahusiano kwa nyakati tofauti ya kimapenzi na Iddy bila ya wao kufahamiana.

Alisema Iddy baaada ya kuingia ndani, 
alimlazimisha msichana huyo kufanya mapenzi na Zuberi huku akimrekodi picha za video kupitia simu yake ya mkononi na baadaye kuzisambaza kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Kamanda Matei alisema watuhumiwa walimtishia kwa kisu msichana huyo asipige kelele wakati akifanyiwa kitendo hicho na kumtaka asitoe siri hiyo vinginevyo atauawa. Baada ya kitendo hicho, imeelezwa kuwa vijana hao walitoweka na baadaye zilionekana picha za msichana huyo akifanya ngono na Zuberi.

Inadaiwa baada ya picha hizo za ngono kumfikia mama yake , alikazimika kumwita binti yake na kumuuliza na akakiri kufanyiwa vitendo hivyo kwa kutishiwa maisha yake endapo angetoa siri.
Mama wa msichana hiyo alilazimika kwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Dakawa , Mei 4, mwaka huu na msako dhidi ya vijana hao ulifanyika na kukamatwa kila mmoja alikokuwa.
Kamanda Matei alisema kuwa, baadaye picha hizo za ngono zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na uchunguzi uliofanyika ulifanikisha kukamatwa kwa watu wengine tisa wa eneo la Dakawa.

Wengine tisa ambao wanakabiliwa na kosa la kusambaza picha za utupu ( Ponografia ) chini ya Kifungu cha 14 (1) (a) cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 ni Rajabu Salehe (26), Said Athuman (26), Musini Ngai (36), Said Mohamed (24) na Hassan Ramadhan (27).

Wengine ni Ramadhan Ally (26), Lulu Peter (38) na Magreth Njonjome (30), ambao wote ni wakazi wa kata ya Dakawa, wilayani Mvomero. “

 Tumeweza kukamilisha uchunguzi wa awali na kuwakamata watuhumiwa 11 , wawili ni waliohusika na vitendo vya ubakaji na wengine tisa kwa kusambaza picha za video kwenye mitandao ya kijamii na tunawafikisha mahakamani kesho (leo),” alisema Kamanda Matei.

Kifungu cha 14 (1) cha Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao kinasema kuwa: “Mtu hatachapisha au kusababisha kuchapishwa kupitia katika mfumo wa kompyuta- ponografia au ponografia yoyote iliyo ya kisherati au chafu.

Kifungu cha 14(2) cha Sheria hiyo kinasema: Mtu atakayekiuka Kifungu kidogo cha ( 1) atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika, iwapo ni uchapishaji kuhusiana na (a) ponografia, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba au vyote kwa pamoja ; au (b) ponografia iliyo ya kisherati au chafu, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni thelathini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka kumi au vyote kwa pamoja”.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!