WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imebaini kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya ramani ya Tanzania ambayo mipaka yake imepotoshwa.
Upotoshwaji huu umefanywa kwenye “diary” (vitabu vya kumbukumbu na matukio), Kalenda, mabango, matangazo ya kwenye vyombo vya habari na sehemu nyinginezo.
Jambo hilo la kupotosha mipaka ni hatari kwa usalama wa nchi.
Ramani sahihi ya Tanzania inatakiwa kuonesha mpaka kwa sehemu ya maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ukipita katikati ya maziwa hayo.
Hivi karibuni tumebaini matumizi ya ramani ya Tanzania kwenye majarida, magazeti na hata Luninga inayopotosha mpaka kwa sehemu ya ziwa Nyasa ikionesha mpaka kupita pembezoni mwa ziwa.
Kitendo cha kuchapisha ramani yenye makosa kwa kutumia vyanzo visivyo rasmi ni kosa kwa mujibu wa mamlaka (Instrument) ya Mhe. Waziri aliyepewa dhamana ya kusimamia sekta ya ardhi ikiwemo masuala ya upimaji na ramani.
Idara ya Upimaji na Ramani ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuandaa, kuchapisha, kutunza na kusambaza ramani zote nchini ipo tayari kutoa ramani kwa matumizi yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na ushauri kuhusu usahihi wa ramani kabla ya kuitumia.
No comments:
Post a Comment