UMBALI wa mita chache kutoka Ofisi za mkuu wa Mkoa wa Njombe,Utakutana na Maporomoko mazuuri na ya kuvutia ya Mto Luhuji.Yapo jirani kabisa na njia panda ya barabara inayokwenda wilayani Makete.
Ukiwa katika njia panda hii kwa harakaharaka ukiangalia upande wa kushoto kwa kupenyeza macho kwenye miti aina ya mikaratusi waweza jua upande wa bondeni kuna paa lililoezekwa bati jipya hivi karibuni.Hii ni kutokana na mng’ao utakaouona. Lakini ukiyapa nafasi masikio yako utaweza kubaini mvumo wa maji yanayotiririka kwa kasi. Wakazi mkoani hapa wanasema Maporomoko haya ya asili ni ya enzi na enzi na yamekuwa yakidumu kwa kipindi cha mwaka mzima japo katika kipindi cha mvua nyingi huongezeka mara dufu.
Maji ya mto Luhuji yalipo maporomoko hutiririkia kwenye mto Ruaha Mkuu. Uwepo wa Maporomoko haya jirani kabisa na mji wa Njombe ni kivutio tosha na fahari kwa wakazi wa mji huu na mkoa kwa ujumla.Kwa waliozoea maeneo ya aina hii kufanyia pikiniki na mapumziko mengine wayaonapo haya hutamani kuhamia Njombe ama kuyahamishia sehemu wanakoishi jambo ambalo ni vigumu kutokea. Lakini kama wahenga walivyosema Palipo na Miti hapana wajenzi.
Eneo la maporomoko ya Mto Luhuji halijaendelezwa kiasi cha kuwa kivutio zaidi cha sekta ya Utalii.Uwe wa ndani au nje. Ni vigumu kuamini nikuambiayo lakini ukweli ndiyo huu.Wapo baadhi waliogeuza eneo hili ni Nyumba ya kulala wageni kwa muda kwa kutumia sehemu ya vichaka kufanyia ngono.Hili utalibaini pale unapofika na kukutana na mipira(Kondomu) zilizotumika. Wapo pia wanaotumia vichaka vya eneo hili kama vyoo.Si kwa haja ndogo tu,bali ukifika utakutana na vinyesi.
Usipokuwa makini waweza kujikuta umechafua viatu vyako kwa kukanyaga vinyesi kwani hata katika njia za kuyaendea maporomoko vipo. Yaanai wapo wakazi wasio wastaarabu ambao huamua kutimiza haja zao njiani na kasha kuendelea na safari zao. Ukiwa kwenye maporomoko haya utajionea piaa baadhi ya wakazi wakitumia sehemu ya mto huu jirani na maporomoko kusafisha pikipiki na baiskeli zao.Maji wanayosafishia vyombo hivi vya usafiri hutiririkia mtoni na kuungana na maji yanayoporomoka.
Shughuli hizi zote zisizo rasmi zinaonesha uwepo wa baadhi ya wakazi wasiotambua umuhimu wa Urithi huu uliopo.Ni nadra kwa mtu anayetambua utalii wa maporomoko makubwa kama haya akaenda kujisaidia haja kubwa au ndogo maeneo ya jirani.Ni vigumu pia mtu kama huyo kukuta akifua au kusafisha vyombo vya usafiri jirani na urithi kama huu. Hivi karibuni wanahabari kutoka Chama cha waandishi wa habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania(TAJATI) walitembelea mkoa wa Njombe.
Miongoni mwa vivutio vya utalii walivyotembelea ni pamoja na Maporomoko haya yam to Luhuji.Hapo ndipo walipojionea tamu na chungu ya eneo hilo muhimu. Awali ilikuwa vigumu kwao kupata njia ya kuelekea yalipo maporomoko wakitokea barabara kuu ya Iringa-Njombe.Hii ni kutokana na kutotengenezwa kwa njia maalumu. Lakini wakiwa katika njia ndogo wakapata wakati mgumu kwakuwa walilazimika kuruka vinyesi walivyokutana navyo.
Lakini wanahabari hawa wakajikuta wanayasahau machungu haya yote baada ya kufikia eneo la maporomoko. Muonekano wa maji yanayotiririka kwa kasi yakiwa yamesambaa juu ya mwamba mithiri ya paa la nyumba ilikuwa kivutio tosha kwao kama wadau wa sekta ya utalii nchini. Maji yanayotiririka hapa hutengeneza manyunyu ambayo huruka kwa takribani umbali wa mita 15 hivyo kusababisha eneo la jirani kuwa na umajimaji wakati wote.
Kutokana na hali ya hewa ya mkoa wa Njombe kuwa ya baridi,manyunyu haya pia huwa ya baridi kiasi cha kumvutia mtu aliyetembea kwa umbali mrefu juani. Hakina yanavutia. Madhari nzuri ya kupigia picha hasa unapopanda katika magogo makubwa ya miti yaliyopo jirani na maporomoko haya yanakufanya ujikute unapiga picha nyingi zaidi za ukumbusho.Yapo pia mawe makubwa ambayo ni kivutio kingine.
Lakini kwakuwa kinachoonekana kukosekana hapa ni uwekezaji ambao unaweza kuleta mwonekano bora zaidi,TAJATI ikaona kuna haja kwa wadau nchini kuhamasishwa kuwekeza katika Maporomoko.Hii itawezesha eneo hilo kuwa kivutio kikubwa cha utalii katika ukanda wa mikoa ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania. Mwenyekiti wa TAJATI Ulimboka Mwakilili alisema ipo haja ya wadau kwa kushirikiana na serikali mkoani hapa kuboresha kivutio hicho ili kiweze kuwa sehemu ya mapumziko ya wageni na wenyeji mjini hapa.
Miji mingi imekosa maeneo ya kupumzika kutokana yaliyo ya kuvutia.Kwa Njombe wana bahati kubwa ya kupata mandhari haya ya asili. “Akija mwekezaji akaboresha mahali hapa,patakuwa na mvuto zaidi na kila mmoja atatamani kuja.Anaweza kuboresha njia,sehemu za kukaa na pia akapanda mimea kama maua yenye kuvutia.Nina hakika maharusi watakuja kupigia picha hapa,na pia shughuli nyingine mbalimbali zitafanyikia hapa.”
Mwakilili anasema kwa kuboreshwa kivutio hicho serikali pia itaweza kujipatia kodi kutokana na watalii wa ndani na nje watakaofika kwenye maporomoko na kulipia kiasi cha fedha kwaajili ya utalii wa eneo hilo.
“Kwa kuachwa namna hii ni dhahiri kuwa serikali inaendelea kupoteza mapato.Iwapo pataboreshwa hapa panaweza kuwa sehemu ya vyanzo vya mapato kupitia utalii” “Kuboreshwa pia kutasaidia utunzaji wa mazingira tofauti na ilivyo sasa.Tumeona watu wanatumia vichaka vya jirani kama vyoo.Hii inasababisha baadhi ya watu kutofika eneo hili kutokana na uchafu unaoonekana ikiwemo vinyesi” anasema Mwakilili.
Katibu wa TAJATI Venance Matinya anasema uwekezaji katika maporomoko haya ni jambo linalowezekana kwakuwa halihitaji kuwekeza fedha nyingi kama ilivyo kwa maporomoko ya kutengenezwa.Haya ni ya asili hivyo uboreshaji ni kidogo sana katika mazingira ya jirani tu. Mmoja wa wanahabari mkoani Njombe Mercy Sikabogo anasema wanahabari wana jukumu kubwa pia la kuihamasisha jamii kulitunza eneo hilo ambalo ni urithi wa kipekee kwa wakazi wa mji wa Njombe na mkoa kwa ujumla.
“Ni imani yetu kuwa kwa TAJATI iliyojikita katika masuala ya Utalii na uwekezaji nchini kulifikia eneo hili,ni mwanzo mzuri wa kujulikana kwa kivutio hiki muhimu.Yawezekana wapo watalii ambao wangependa kutembelea maeneo kama haya lakini hawajui iwapo na hapa Njombe kuna fursa hii” “Iwapo kukawa na mikakati ya pamoja baina ya wadau mbalimbali watakaoshirikiana na Tajati,serikali ya mkoa na halmashauri kupitia ofisi za Maliasili,Utalii na utamaduni kivutio hiki kitakuwa chanzo kikubwa cha mapato katika miaka michache ijayo.
Na watu watastaajabu kuona eneo waliloliona la kawaida kwa muda mrefu linakuwa chachu ya maendeleo” Mercy anawasihi wawekezaji walio na mwamko juu ya masuala ya utalii kuja kuwekeza kwa kuweka miundombinu itakayowashawishi watalii wa ndani na nje kutembelea eneo hilo.Na si kwa utalii pekee hata kwa uzalishaji nishati muhimu ya umeme.Maporomoko haya yanaweza kutumika kuzalisha nishati hiyo na kuuwezesha mji wa njombe kuondokana na utegemezi wa umeme kutoka Gridi ya Taifa.
Saspedo Mazengo,ni kijana mkazi wa njombe ambaye wanatajat wakiwa wanatoka eneo hili walikutana nae akiwa ameongozana na binti mmoja kuelekea kwenye maporomoko.Yeye pamoja na mwenzie walijitambulisha kuwa watalii wa ndani wanaopenda kutembelea eneo hilo.
“Huku Njombe hatuna Beach kama ilivyo kwa wakazi wa mikoa ya pwani na maeneo yaliyo na maziwa. Maporomoko haya kwangu naona kama sehemu ya kuja kutuliza mawazo. Lakini mandhari bado hayavutii.Tunahitaji wawekezaji kuboresha eneo hili. Walau viwepo vinywaji vinavyouzwa hapa na kuongezwa kwa nakshi za mimea ya kuvutia. Hii itakuwa safi sana.”
No comments:
Post a Comment