Sumbawanga. Mkazi wa kijiji cha Chala B, Tarafa ya Chala wilayani Nkasi, Rukwa Moses Nambasita (48) ameuawa kinyama kwa kuchomwa visu mwili mzima kutokana na kinachodaiwa kuwa wivu wa kimapenzi.
Akisimulia mkasa huo Mwenyekiti wa kitongoji hicho Vicent Mwanambuu alisema kuwa tukio hilo limetokea jana saa 10 jioni ambapo marehemu alivamiwa na Peter Kiberenge (45) alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda nyumba ya jirani ambapo alishambuliwa kwa kuchomwa visu.
Alisema kuwa kuwa baada ya yeye kupata taarifa hizo alitoa taarifa katika kituo kidogo cha polisi Chala na walifika na kuichukua maiti hiyo kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi na kuanza kumsaka mtuhumiwa
Akielezea chanzo cha mauaji hayo, Mwanambuu alisema Kiberenge alipata taarifa kuwa marehemu ana mahusiano na mtalaka wake ambaye walikuwa wameachana kwa kipindi kirefu.
Alidai kuwa kutokana na taarifa hizo mtuhumiwa alipeleka shauri hilo la ugoni katika mahakama ya Mwanzo Chala.
“Lakini kabla hata shauri hilo halijamalizika, tunashangaa kuona kuwa mtuhumiwa huyo ameamua kujichukulia sheria mikononi na kuwa baada ya kutekeleza unyama huo alikimbia na kuelekea kusikojulikana,” alisema
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Godfrey Mwanakatwe alidai kuwa kutokana na mazingira hayo jeshi la polisi linawashikilia watu wanne kwa kosa la kushiriki katika mauaji hayo, baada ya wao kutoa taarifa kwa muuaji kuwa marehemu ana mahusiano ya kimapenzi na mtalaka wake huyo ambaye hata hivyo naye mpaka sasa haijulikani alipo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema baada ya uchunguzi wa polisi ndugu wa marehemu waliruhusiwa kuuzika mwili huo huku jamii hiyo ikipewa elimu juu ya watu kuacha kujichukulia sheria mikononi.
Alisema chanzo cha kifo hicho ni wivu wa kimapenzi na kuwa mtuhumiwa alianza vizuri kufuata sheria kwa kwenda mahakamani lakini haijulikani nini kilichomfanya tena kuchukua maamuzi hayo ya kinyama.
Alisema wanaoshikiliwa na polisi hadi sasa ni Mzee Ezebius (66),Revocatus Kiberenge(23),Giles Kiberebge (36) hao wote wanatuhumiwa kushiriki katika mauaji hayo kwa kutoa taarifa kwa mtuhumiwa aliyetekeleza mauaji hayo (Peter Kiberenge) kuwa marehemu ana mahusiano ya kimapenzi na mke wake huyo ambaye waliachana muda mrefu.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment