Friday, 29 April 2016

MAFURIKO YAUA 13 NA KUATHIRI WENGINE 13, 933 MOROGORO


WATU watano wamefariki dunia na wengine 13,933 kutoka kaya 3,095 wameathiriwa baada ya kutokea kwa mafuriko makubwa ya mvua zilizonyesha maeneo mbalimbali ya wilaya za Kilosa, Kilombero, Morogoro na Wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro.


Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Steven Kebwe alisema hayo jana wakati akitoa taarifa ya awali ya mafuriko yaliyotokea mkoani humo kutokana na mvua zilizonyesha Aprili 23 na 24, mwaka huu.
Dk Kebwe alisema mbali na kusababisha vifo vya watu watano, pia mvua hizo zimesababisha madhara makubwa kwa wananchi kwa kuharibu mali, mazao mashambani na miundombinu ya barabara na hivyo kusababisha maeneo mengi kutopitika.
Alisema kutokana na mafuriko hayo, kaya 3,095 zenye wakazi 13,933 zimeathiriwa ikiwemo kubomoa jumla ya nyumba 315 na kuharibu mashamba hekta 12,073 kutoka katika wilaya za Kilosa, Kilombero, Morogoro na Malinyi.
Alizitaja wilaya ambazo mafuriko ya mvua yalisababisha vifo ni Kilombero kwa watu watatu wakiwemo wanafunzi wawili wa shule za msingi waliokuwa wakivuka mto Lumemo na mmoja wakati akivuka mto eneo la Kisawasawa.
Kwa wilaya ya Morogoro, watu wawili walifariki dunia Aprili 23, mwaka huu akiwemo mwanamume dereva wa gari la kukodishwa ambaye ni mkazi wa Ngerengere aliyezama alipokuwa akivuka mto Ngerengere.
Mbali na huyo, pia mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 10 alizama maji kwenye mto Mvuha baada ya gema la mto kukatika. Mtoto huyo alikuwa amekaa pembezoni wakati mama yake akiosha vyombo karibu na mto huo.
Dk Kebwe alitaja madhara mengine kutokana na mafuriko kwa wilaya hizo ni Kilosa katika vijiji vitano kaya 1,238 zenye idadi ya watu 4,765 zimekumbwa na athari za mafuriko ikiwamo kuharibu nyumba 1,120 na kubomoa 144.
Halmashauri ya wilaya ya Morogoro, ilikumbwa na janga hilo Aprili 23, mwaka huu katika vijiji 14 kutoka kata za Serembala, Mvuha, Tununguo na Mkulazi ambako wakazi 8,795 walio katika kaya 1,759 waliathiriwa na mafuriko.
Kwa wilaya ya Malinyi kutokana na mvua zilizoanza kunyesha Aprili 10 hadi 26, mwaka huu, zimeharibu vibaya barabara nyingi ikiwemo ya Lupiro – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo kilometa 94.
Pia alitaja athari nyingine zilizosababishwa na mafuriko hayo ni kufungwa kwa Shule ya Msingi Ngombo kuanzia Aprili 12, mwaka huu hadi sasa kutokana na kuzingirwa na maji. Dk Kebwe pia alisema katika wilaya hiyo, jumla ya hekta 6,000 za mpunga, mahindi na ufuta zimesombwa na maji katika vijiji vya Usangule, Ngoheranga na Biro.
“Wilaya ya Ulanga, Gairo na Mvomero pamoja na kupata mafuriko, lakini hakuna madhara makubwa yaliyojitokeza mpaka sasa,” alisema Dk Kebwe. Alisema Morogoro ni kati ya mikoa 10 iliyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kuwa itakuwa na mvua nyingi katika kipindi hicho na kutokana na mafuriko hayo, hali ya barabara si ya kuridhisha katika maeneo mengi baada ya kuharibiwa na mvua.
Aliwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia kwa kutoa vyakula na misaada mingine ya kibinadamu kwa ajili ya kuwapatia wale walioathiriwa wakiwemo na wananchi wenye mapenzi mema. Alisema tayari Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeahidi kutoa dawa za kutosha kukabili magonjwa ya mlipuko.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!