Friday, 29 April 2016

Magufuli amtumbua aliyesusa mshahara wa 180m/-

RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Julieth Kairuki, kuanzia Jumapili iliyopita, kutokana na kutochukua Sh. milioni 180 za mishahara kwa miaka mitatu.





Hatua hiyo imechukuliwa na kutangazwa siku chache baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Ally Simba.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof. Adolf Mkenda, Rais Magufuli alitengua uteuzi huo baada ya kupata taarifa kuwa, Kairuki hajachukua mshahara wa serikali tangu alipoajiriwa Aprili 2013.
Ingawa taarifa ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji haikutaja kima cha mshahara cha Mkiurugenzi Mtendaji huyo wa TIC wala jumla ya fedha ambazo Kairuki alistahili kulipwa kwa kipindi hicho, lakini habari zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii kwa kutwa nzima ya jana, na taarifa za kuaminika kutoka ndani ya TIC zilizopatikana jioni, zilieleza kuwa Kairuki alistahili kulipwa Sh. milioni tano ( 5) kwa mwezi.
Hata hivyo, kwa kipindi cha miaka mitatu ambacho Kairuki alikuwa mkuu wa kituo hicho cha kuhamasisha uwekezaji kitaifa na kimataifa, Mkurugenzi huyo hakupokea mshahara wake kwa sababu ambazo taarifa pia haikuweka wazi.
Uteuzi wa Kairuki ulianza Aprili 12, 2013, taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ya Aprili 22, mwaka huo ilisema; akichukua nafasi ya Emanuel Ole Naiko ambaye alistaafu.
"Kairuki ni Mwanasheria mwenye Shahada ya Kwanza na ya Uzamili kwenye Sheria, " taarifa hiyo ilisema na kueleza zaidi kuwa, "ni mtaalamu wa miradi ya ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PP)."
Kabla ya kujiunga na TIC, Kairuki alikuwa Meneja wa Mradi wa Kujenga Uwezo wa PP kwa nchi za SADC katika Chama cha Mabenki ya Afrika Kusini kati ya mwaka 2002 hadi mwaka 2008.
Mwaka 2008 hadi mwaka 2013, Kairuki alikuwa Meneja Mkuu wa Idara ya Benki na Huduma za Fedha katika taasisi hiyo ya mabenki.
Kwa mujibu wa sheria ya PPP ya mwaka 2010, TIC ndio msajili wa miradi ya ubia wa PPP na mtathmini wa chambuzi yakinifu katika miradi ya namna hiyo inayokuja nchini.
Nay Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya TIC aligoma kuzungumzia suala hilo alipoombwa kutoa ufafanuzi jana.
Katibu Prof. Mkenda, alipoulizwa na Nipashe mshahara halali ambao serikali ilipanga kumlipa lakini Kairuki hakuuchukua, alisema hawezi kuuzungumzia.
Alisema sababu ya kushindwa kueleza kiwango cha mishahara yake aliyogoma kuichukua ni kutokana na kuchukuliwa maamuzi na ngazi za juu, na kwamba bado ni mtumishi wa serikali.
Prof. Mkenda ambaye alijibu swali hilo kupitia msemaji wa TIC, Edward Mkomola, alisema Kairuki bado ana nafasi ya kufanya kazi serikalini baada ya uteuzi wake kutenguliwa endapo atakubali kufanya kazi nyingine atakayopangiwa.
Kairuki alipoitafutwa ili kuthibitisha mshara unaotajwa kama ndio alioukataa, simu yake iliita bila majibu.
VIATU VIKUBWA?
Kwa upande wake Mhadhiri na Mtafiti wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Haji Semboja alisema utenguzi unaoendelea huenda unatokana na wahusika kuonekana wamewekwa kwenye nafasi ambazo sio zao.
Alisema kuacha kupokea mshahara sio jambo rahisi; huenda Kairuki alikuwa na sababu za msingi za kuacha kuupokea mshahara huo.
“Huenda alikuwa na marupurupu yanayomtosheleza. Naweza nikasema huenda ana fedha akaamua kuacha kupokea akijua atakuja kupatiwa, hayo ni malengo ya mtu na isitoshe yule hana shida ya fedha," alisema Profesa Semboja.
“Labda tujiulize alikuwa akisafiri kwa kutumia hela yake mwenyewe ama ni ya serikali?”
Kwa nafasi yake, Kairuki alikuwa katika nafasi ya kusafiri mara kwa mara.

Alisema Kairuki hakuwa na shida tu ya kuongezwa mshahara kwani alikuwa na uwezo wa kifedha, "hivyo sidhani kama alikuwa na shida ya mshahara.
“Kumuondoa kazini kwa sababu ya mshahara sijaona kama ni 'issue' 9hoja ya msingi) waliomuajiri kwa muda nao wangeondolewa, ikiwemo na bodi na hata Waziri angewajibishwa maana kwa sasa imekuwa ni fasheni kuwaondoa (watumishi)kazini.”
Profesa Semboja alisema uchumi wa nchi hauwezi kukua kwa kufukuzana na jambo la msingi linalotakiwa kuangaliwa ni namna ya kupata maendeleo.
Imeandikwa na Beatrice Shayo na Mary Geofrey

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!