Sunday, 20 March 2016

TMA YATAHADHARISHA KUHUSU JOTO KALI

Mamlakaya Hali ya Hewa (TMA), imesema utabiri unaonyesha kiwango cha juu cha joto leo kitafikia nyuzi joto 36 katika mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro huku Dar es Salaam na Tanga kikiwa ni 35 hivyo imewashauri wananchi kutumia mbinu za kawaida za kujikinga na joto linaloendelea.
 
Katika taarifa yao waliyoisambaza jana kwenye vyombo vya habari, TMA ilikanusha uvumi wa kwenye mitandao ya kijamii uliodai kiwango cha juu cha nyuzi joto leo kitafikia nyuzi joto 40.
 
Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa TMA, Dk. Pascal Waniha aliliambia gazeti hili kuwa, kiwango cha juu cha nyuzi joto kama hicho cha 36 kiliwahi kutoka miaka ya nyuma kwenye miji ya Moshi na Dar es Salaam. 
 
Taarifa ya TMA ilisema katika mji wa Moshi kiwango cha chini cha joto kitakuwa ni 20 wakati Dar es Salaam kitakuwa 26 na Tanga 25.
 
Taarifa hiyo ilisema  Zanzibar  itakuwa na kiwango cha juu cha joto 34 na cha chini 26.
 
“Mji wa Dodoma utakuwa na kiwango cha juu cha joto 32 na cha chini kitakuwa 20 na kufuatiwa na mji wa Tabora utakaokuwa na kiwango cha juu cha 31 na cha chini 19,”  ilisema.
 
Aidha, taarifa ilisema miji ya Iringa na Kigoma kiwango cha juu cha joto kitakuwa ni 30 na cha chini (Kigoma 21 na Iringa 15).
 
“Mji wa Arusha kiwango cha juu kitakuwa 29 na cha chini kitakuwa  17 na kufuatiwa na Mwanza  ambapo cha juu ni 28 na cha chini ni 20 wakati mji wa Mbeya kiwango cha juu kitakuwa ni 27 na cha chini 13,” ilisema taarifa hiyo.
 
Ilisema ongezeko hilo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na ongezeko la joto katika eneo la kati ya bahari Kuu za Hindi na Pasifiki (uwepo wa El Nino) na kwamba wanatarajia mabadiliko kidogo na ya kawaida katika hali ya joto iliyopo sasa.
 
TMA ilisema kumekuwa na mkanganyiko katika jamii kutokana na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii juzi kuwa hali ya joto na kuihusisha na tukio linalotarajiwa la jua la utosi kuwa kwenye mstari wa Ikweta leo.
 
Taarifa ilifafanua kuwa matukio ya jua kusogea karibu zaidi na uso wa dunia ni jambo la kawaida hutokea mara mbili kwa mwaka miezi ya Machi na Septemba.
 
“Kutokana na njia ambayo dunia hutumia kulizunguka kitaalam hali hiyo inajulikana kama ‘Equinox’ ni kweli kwamba katika kipindi hicho joto katika uso wa dunia linatarajiwa kuwa kubwa katika maeneo ya Ikweta kwa sababu ndicho kipindi pekee ambacho jua lipo karibu na uso wa dunia, lakini hakuna ukweli wowote kuwa joto litafikia nyuzi joto 40 mahali popote Tanzania kama taarifa za mitandao zilivyoeleza,’ ilisema taarifa.
 
Taarifa ilisema kinachotarajiwa leo ni nyuzi joto 36 katika mji wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!