Sunday, 20 March 2016

MAKONDA KUIBADILISHA DAR ES SALAAM


Siku chache baada ya kuapishwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekuja na mikakati tisa ikilenga kubadilisha mwonekano wa jiji hilo na kulifanya liwe la kisasa.
Miongoni mwa mambo aliyoyagusia ni usafi, ofisi za Serikali kutokuwa za chama, kutenga maeneo ya biashara, sensa ya nyumba kwa nyumba, usalama wa raia na mali zao, watumishi hewa, kurudisha hadhi ya watendaji wa Serikali za Mitaa, elimu na barabara.


Alitoa mikakati hiyo jana alipokuwa akizungumza na wenyeviti na watendaji wa mitaa 559 ya jiji la Dar es Salaam katika mkutano wa kujitambulisha kwao.
Usafi
Kuhusu usafi, Makonda alitangaza zawadi ya gari la Sh20 milioni au fedha taslimu kwa mwenyekiti ambaye mtaa wake utaongoza kwa usafi na Sh5 milioni kwa kila mjumbe wa mtaa husika. Zawadi hiyo itakayokuwa ikitolewa kila baada ya miezi mitatu, itaanza rasmi Aprili Mosi.
Pia, aliahidi kutoa pikipiki 30 kwa Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam ili kuwawezesha askari kuwafuatilia watu watakaotupa taka ovyo barabarani.
“Kampeni ya kushindanisha mitaa bora kwa usafi itaanza kutakuwa na utaratibu wa kukutana na viongozi kwa ajili ya kujadiliana mambo mbalimbali ikiwamo kukabidhi zawadi kwa mwenyekiti atakayeibuka mshindi,” alisema.
Ofisi za Serikali kuwa za chama
Mkuu huyo wa mkoa ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, alisema ofisi za Serikali ni kwa ajili ya kazi na siyo sehemu ya kufanyia siasa akisema katika uongozi wake haangalii chama, bali kusikiliza matatizo ya kila mtu.
“Ninyi ni kama viongozi wengine, nataka mtimize ahadi zenu mlizowaahidi wananchi kipindi cha kampeni siyo kuleta siasa. Tushirikiane kuleta maendeleo katika jiji hili linalotazamwa na kila mtu,” alisema.
Kutenga maeneo ya biashara
Makonda alisema matamanio yake ni kuiona Dar es Salaam ya kisasa ambayo itakuwa na maeneo maalumu kwa ajili ya biashara ya vileo, magari, gereji na vifaa vya ujenzi.
“Ninatamani kuona Wilaya ya Kinondoni, Ilala na Temeke zikitenga maeneo maalumu kwa ajili ya maduka ya magari na gereji pia.”
Aliwaagiza wakurugenzi wa manispaa ifikapo Mei Mosi wawe wameainisha maeneo maalumu kwa ajili ya biashara hizo, huku akitoa mwaka mmoja kwa wafanyabiashara husika kuhamia huko.
“Kingine wenyeviti kuanzia sasa ni marufuku maeneo ya pembezoni mwa barabara watu kufanya biashara ikiwamo Ubungo,” alisema Makonda.
Alisema wanaofanya biashara katika maeneo hayo wamekuwa hawalipi kodi hali inayowaumiza wafanyabiashara wa maeneo rasmi na Serikali kukosa mapato.
Alisema baadhi ya watu wanaofanya biashara katika maeneo hayo wanashirikiana na wenyeviti wa Serikali za Mitaa husika.
Wakati akiendelea kuzungumzia suala hilo, mmoja wa mwenyekiti alisimama na kutaka kumpa taarifa lakini Makonda alimkatisha akisema: “Mkuu wa mkoa akiongea hakuna taarifa, halafu mimi ni mdogo kwenu lakini ndiyo hivyo kiongozi wenu.” Kisha aliendelea bila ya kutoa fursa hiyo.
Alisema atazungumza na wakurugenzi wa manispaa kuangalia namna ya kuandaa utaratibu wa kutenga barabara moja kwa kila kata kwa siku moja ili watu wafanye biashara.
Sensa nyumba kwa nyumba
Makonda aliwataka wenyeviti hao kupita kila nyumba katika mtaa kuorodhesha idadi ya watu wanaoishi na shughuli zao.
“Kwa kuwapitia nyumba kwa nyumba mtajua watu na shughuli zao hata kuwabaini wahalifu. Hao ndiyo tunaowatafuta, msiwavumilie watoeni msiogope kufa kwa kuhofia kuwataja.”
Alisema hiyo itasaidia pia kujua watu wasiokuwa na ajira hivyo kujipanga namna ya kuwasaidia.
Usalama wa raia na mali zao
Makonda alisema kila mwenyekiti wa mtaa anapaswa kuhakikisha wananchi wake wanakuwa salama na hilo litafanikiwa endapo atakuwa na utaratibu wa kujua nani anafanya nini.
Aliahidi kutoa Sh1 milioni kwa polisi atakayepambana na majambazi, huku milioni moja nyingine ikienda kwa mtu atakayesalimisha bunduki au bastola kituo cha polisi.
Watumishi hewa
Akizungumzia watumishi hewa, alitoa agizo: “Nitakapoagiza orodha ya watumishi hewa ije kamili, kinyume na hapo ofisa utumishi atalazimika kulipa hata madeni yaliyopita maana anaonekana ana nia ya dhati ya kufuga uozo huo.”
Hadhi ya watendaji wa mitaa
Makonda pia aliwaahidi kuwajengea ofisi wenyeviti wote wa Serikali za Mitaa na kuachana habari za kupanga na kwamba ifikapo Aprili Mosi atawakopesha pikipiki 1,000 ili ziwasaidie katika utendaji wao wa kazi na kuwasaidia kujikimu kimaisha.
“Kuanzia sasa, hakuna mtu kwenda kumuona mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa bila kuanzia kwa mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa husika ili kurejesha heshima ya viongozi hawa.”
Elimu
Katika elimu aliwataka watendaji na wenyeviti katika mitaa yao kutafuta wadau kusaidia sekta hiyo badala ya kusubiri Serikali.
Barabara
Kuhusu kero ya barabara, aliahidi kuzishughulikia, huku akiwashangaa wahandisi kwa kukaa ofisini.
Mtazamo wa wenyeviti
Wakizungumzia maagizo hayo, baadhi ya wenyeviti na watendaji walisema mengi yanaweza kutekelezeka kwa kuwa mkuu wa mkoa ameonyesha nia katika kuhakikisha jiji linabadilika.
“Mengi aliyoyaongea yalikuwa yanafanyika lakini tulikuwa tunakosa msukumo kutoka juu. Kama ameonyesha nia, hatuna budi kumuunga mkono na kuifanya Dar es Salaam kuwa mji wa aina yake,” alisema Mwenyekiti wa Mtaa wa Faru – Buguruni, Simba Said.
Mwenyekiti wa wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Ubaya Chuma alisema watendaji wa ngazi za mitaa wamekuwa na mengi ya kufanya lakini hawakuwa na fursa hivyo ujio wa Makonda huenda ukaleta mabadiliko.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!