“UDUMAVU wa mwili na akili unaosababishwa na ukosefu wa chakula cha kutosha, unaathiri sana elimu katika mkoa wa Dodoma.”
Maneno hayo yanasemwa na Ofisa Elimu Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda wakati wa mahojiano na mwandishi wa makala haya. Mkoa wa Dodoma unakabiliwa na tatizo la udumavu kwa kiwango cha asilimia 56 ukilinganisha na asilimia 42 ya kitaifa, kutokana na kukosekana kwa lishe bora kwa mama anapopata ujauzito, hadi mtoto anapokua na hata utu uzima wake.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa, mkoa wake una udumavu mbaya zaidi kwani unahusisha akili. “Udumavu wa akili ni mbaya sana kwani mikoa mingine ina ukondefu na udumavu wa misuli ambao unaweza kurekebishika lakini udumavu wa akili hauwezi kurekebishika. Tunaomba mkoa wa Dodoma upewe kipaumbele katika kukabiliana na tatizo hilo,” anasema.
Anasema bila kupambana na umaskini kuanzia ngazi ya kaya tatizo la udumavu litaendelea kuleta athari kubwa katika maisha ya kila siku ya watoto. Pamoja na tatizo la udumavu kuathiri elimu, changamoto nyingine za elimu katika mkoa wa Dodoma zinatajwa kuwa ni mkoa kushika nafasi mbaya kitaifa katika mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne, upungufu wa madawati, matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na wanafunzi wengi kuacha shule kutokana na sababu mbalimbali.
Kaponda anasema tatizo la udumavu linaathiri maendeleo ya elimu kwa kiwango kikubwa, hali inayofanya kila mwaka ufaulu kuwa duni. “Bora mtoto ale hata mchana, usiku asile lakini kwenye maeneo mengine watoto hawapati chakula kabisa hata unapomfundisha ubongo unakuwa umelala, chakula cha ubongo ni glucose (sukari) na starch (wanga), mtoto vyote havipati,” anasema.
Anasema mtoto anaweza kulala na njaa na asubuhi analazimika kwenda shuleni, hivyo anapofundishwa ni vigumu kuelewa na hivyo ni vyema angalau saa nne apate uji akiwa shuleni. Kaponda anasema shida iliyopo ni wazazi kukwepa majukumu ya msingi na kufanya mambo yasiyo na manufaa sana kama elimu. Anasema harusi na sherehe mbalimbali zimekuwa zikichangiwa fedha nyingi na kupewa kipaumbele lakini ni vigumu watu kuchangia ili kuhakikisha watoto wanapata chakula wakiwa shuleni.
Anasema serikali haiwezi kufanya kila kitu na jamii ambayo watoto wanasoma shule za kutwa inapaswa kujitahidi kuchangia chakula ili watoto wapate uji na chakula wakiwa shuleni kwani inaonesha upatikanaji wa chakula shuleni umekuwa ukiongeza mahudhurio ya wanafunzi. Kaponda anasema dhana ya elimu bure wananchi hawajaipata sawasawa na Februari mwaka huu amepanga kukutana na bodi na kamati za shule ili kueleza nini maana ya elimu bure.
Anasema kinachoonekana sasa watu wameanza kukimbia majukumu wakiambiwa wachangie chakula kwa wanafunzi wa kutwa wanaona kama wanaonewa. Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Vincent Assey anasema madhara ya lishe duni yamekuwa yakichangia kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali na hata kudidimiza nguvu kazi ya taifa kwani watu wenye tatizo hilo wanakuwa na ufanisi duni ikiwemo kuchoka haraka.
“Watoto 42 kati ya 100 wana udumavu wa kimwili na kiakili,” anasema. Celestine Mgoba, Mratibu na taasisi ya chakula na lishe anasema jamii kubwa ya watu, hususani mkoani Dodoma hawali vyakula vyenye virutubisho vya kutosha. “Kama wanakula ni kwa kiwango kidogo. Kaya nyingi zinategemea vyakula ambavyo havibadilishwi. Hula mlo huo huo kila siku,” anasema.
Anasema hali hiyo imekuwa ikifanya watu wengi hasa watoto kukosa madini na vitamini muhimu mwilini. “Asubuhi uji wa mahindi uliokobolewa, mchana ugali na usiku ugali. Jambo kama hilo limekuwa likisababisha watoto kupata madhara yatokanayo na lishe duni,” alisema.
Changamoto zingine za elimu Dodoma
Akizungumza hivi karibuni wakati wa kikao kazi cha watendaji wa sekta ya elimu ngazi ya halmashauri na mkoa, Mkuu wa Mkoa, Chiku Galawa alisema mkoa haujafikia mahali pa kujivuna ama kuridhika katika sekta ya elimu hasa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari kwani haushiki nafasi nzuri za kitaifa kwa darasa la saba na kidato cha nne. Akitoa mfano, anasema mwaka 2014, mkoa ulishika nafasi ya 19 kwa kidato cha nne wakati kwa darasa la saba ukashika nafasi ya 24 kwa mwaka 2015.
Mkuu wa mkoa anasema kumekuwepo na wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika katika shule za msingi ambapo darasa la kwanza ni 110 sawa na asilimia tatu, darasa la nne ni 906 sawa na asilimia mbili, darasa la pili ni 4,290 sawa na asilimia 14 na darasa la kwanza ni 5,066 sawa na asilimia 20. Anasema elimu ya awali haijapewa mkazo unaostahili ambapo katika shule nyingi madarasa ya elimu ya awali, hufundishwa na watu wasiosomea ualimu.
“Mahali pengine hufundishwa kwa bahati tu yaani hakuna mwalimu aliyetengwa kwa ajili yao, watoto hao huishia kucheza tangu asubuhi hadi saa tano au chini ya hapo wanapoondoka. Hilo sio kusudio la serikali,” anasema. Pia anasema kumekuwa na ufuatiliaji duni katika utekelezaji wa elimu ya msingi na sekondari kwani walimu wamekuwa wakifundisha kwa asilimia zisizozidi 40 tu. “Hakuna hatua thabiti zinazochukuliwa kwa walimu wasiowajibika kama utoro wa walimu waliokithiri kwani baadhi ya walimu huwa nje ya vituo vya kazi kwa zaidi ya mwezi,” anasema.
Aidha anasema tatizo lingine ni walimu kwenda masomoni bila vibali, walimu kufundisha bila maazimio wala maandalio kwa mwaka mzima, shule kutokuwa na bodi au kamati za shule za msingi, wakuu wa shule na walimu wakuu kuendesha shule bila vikao vya bodi, kamati za shule na shule kutokaguliwa kwa muda mrefu. Anaitaja changamoto nyingine kuwa ni mashauri ya walimu kuchukua muda mrefu bila kutolewa maamuzi na mamlaka ya nidhamu, yaani TSC, ambapo baadhi ya mashauri huchukua zaidi ya mwaka mmoja bila kutolewa maamuzi.
Akitoa mfano anasema shauri la mwalimu Juma Andallah wa Chamwino ambaye ana shauri la tangu mwaka 2006 lakini hadi sasa halijahitimishwa na wakati mwingine mashauri kama hayo husababishwa na waajiri (wakurugenzi) kutowasilisha TSC mashauri kama hayo kwa wakati. “Tatizo hili linaitia aibu serikali na hivyo walimu wanafanya makosa bila kuogopana kama vile serikali haipo,” anasema.
Anasema tatizo lingine ni kitengo cha elimu ya watu wazima kutowajibika ipasavyo. Akizidi kuorodhesha changamoto, anasema ni ni ugawaji mbaya wa walimu hasa katika shule za pembezoni. Anasema shule hizo zina upungufu mkubwa wa walimu kwani wapya wamekuwa wakipangiwa shule za mijini ama za barabarani.
“Baadhi ya shule zina ziada kubwa sana ya walimu wakati zingine zina upungufu mkubwa na tatizo hili ni kubwa sana kwa shule za msingi kwani walimu wamekuwa wakihamishwa kutoka kwenye shule zenye upungufu mkubwa kwenda kwenye shule zenye walimu wa kutosha na mahali pengine penye ziada,” anasema na kuongeza kwamba halmashauri ya manispaa ya Dodoma ndiyo inayoongoza kwa upangaji mbaya wa waalimu.
Galawa anasema zipo shule nyingi zenye walimu watatu kwa wanafunzi zaidi ya 500, hali hiyo inayochangia kuifanya Manispaa ya Dodoma kuwa moja ya manispaa zinazofanya vibaya sana katika mtihani wa darasa la saba kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo sasa.
Anasemwa mwaka 2015 ilikuwa manispaa ya 28 kati ya 30 zilizofanya mtihani wa darasa la saba. Pamoja na changamoto hizo, anataka kuhakikisha shule zote zinatoa elimu bure na kwamba mwalimu mkuu wa shule yoyote atakayethubutu kuchangisha aina yoyote ya michango atachukuliwa hatua za kiutawala mara tu taarifa zitakapopatikana na kuthibitika. “Pasiwe na michango kwa kupitia milango ya mbele wala ya nyuma” anasema.
No comments:
Post a Comment