Wafanyakazi saba kati ya nane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ambao walitoroka kukwepa tuhumiwa za kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019 kutoka bandari kavu (ICD), wamekatwa na wanaendelea kuhojiwa na polisi juu ya tuhuma hizo.
Watumishi hao ni kati ya watuhumiwa 15 wa TPA waliotangazwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa wameshiriki kutorosha makontena na magari hayo kutoka katika bandari kavu saba bila kulipa ushuru wa Bandari.
Wafanyakazi hao wanatuhumiwa kuipotezea Serikali mapato ya Sh. bilioni 48.55.
Taarifa za kukamatwa kwa watumishi hao zilioenekana kwenye mtandao wa Jamii Forum juzi usiku na baaye kuthibitishwa na Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi, ambaye alikiri kuwa taarifa hiyo imetoka kwenye ofisi yake.
Ruzangi alisema mfanyakazi mmoja hajapatikana na polisi wanaendelea kumsaka ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Wote walishapatikana kasoro mtumishi mmoja, Happygod Naftali, ambaye huyu alishaacha kazi siku nyingi baada ya viongozi kuanza kufuatilia suala hilo. Lakini bado polisi wanaendelea kumsaka,” alisema Ruzangi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kwamba bado wanaendelea kuhojiwa kuhusu tuhuma hizo.
“Tunaendelea na upelelezi wetu lakini idadi nitaitoa siku nitakapozungumza na waandishi wa habari wiki hii,” alisema Sirro ambaye hakutaka kutaja idadi ya wafanyakazi wa TPA ambao wameshapatikana.
Watumishi waliokamtwa na polisi, kwa mujibu wa Ruzangi ni Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet Kimaina, Zainab Bwijo na Nathan Edward.
Watumishi hao wanaungana na watumishi wengine saba John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman (Kova) na Benadeta Sangawe waliokamatwa na kuhojiwa kuhusu sakata hilo.
Watumishi hao saba, kwa mujibu wa Sirro, tayari walishapelekwa mahakamani.
“Ukiacha wale saba ambao tumeshawafikisha mahakamani, hawa wengine bado tuko nao tunaendelea kufanya upelelezi,” alieleza.
Kuhusu mawakala 280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo yao makao makuu ya TPA namna ya walivyohusika kulipia makontena hayo, Ruzangi alisema mamlaka yake inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya suala hilo.
“Tunaendelea kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu mawakala hao, tutatoa taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja Mawasiliano huyo.
Tangu Rais John Magufuli aingie madarakani, uongozi wake umeibua ufisadi wa kutisha ambao ulikuwa unafanywa Bandari ya Dar es Salaama kwa kuwashirikisha wafanyakazi wa TPA na mawakala pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kwa mara ya kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutinga bandarini na kubaini makontena hayo kutolewa bandari kavu bila kulipiwa kodi.
Upotevu huo ulifanya vigogo wa TRA, akiwemo Kamishna Mkuu Rished Bade na makamishna wengine kusimamishwa kazi na wengine kufikishwa mahakamani.
Baadaye Majaliwa alibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila kulipiwa ushuru wa Bandari.
Katika sakata hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya biashara na TPA na sakata la mwisho ni la kupotea kwa makontena 11,019 na magari 2,019 hivyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment