Tuesday 12 January 2016

UCHAGUZI ZANZIBAR KURUDIWA


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amesema uchaguzi mpya utafanyika visiwani humo katika tarehe itakayotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).


Amefafanua kwamba kufanya hivyo ni utekelezaji wa demokrasia, baada ya kufutwa kwa uchaguzi uliofanyika mwezi uliopita.
Akihutubia vijana katika viwanja vya Maisara mjini hapa jana, Dk Shein alisema kwamba baada ya kurekodi ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana, ZEC ilifuta uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba na sheria.
‘’Ni jambo la kusikitisha kwamba baadhi ya watu wanajaribu kutuchelewesha katika uendeshaji mzuri wa demokrasia, huku wakieneza uvumi mwingi dhidi yangu na pia kuyadharau Mapinduzi. Hali hii si nzuri katika juhudi za kuimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU),’’ alisema Dk Shein.
Vijana hao walikusanyika katika viwanja hivyo vya Maisara kuhitimisha Matembezi ya Heshima ya Siku ya Mapinduzi, inayoadhimishwa leo katika Uwanja wa Amani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na viongozi wengine wa CCM, walikuwa ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria hafla ya kuyapokea matembezi hayo.
Matembezi ya kuunga mkono Mapinduzi, hufanyika kila mwaka na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).
Dk Shein aliwapongeza vijana hao kwa kuendeleza matembezi hayo, yanayowakumbusha vijana juu ya majukumu yao katika kuyalinda Mapinduzi.
Mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM, Sadifa Juma na Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja huo, Shaka Hamidu walisema jumuiya yao imekuwa ikifanya kazi kwa bidii, kuhakikisha kwamba demokrasia na Mapinduzi, vinadumishwa kwa amani na kwamba yeyote anayeonesha wasiwasi juu ya mapinduzi, awekwe kando.
‘’Tanzania (ikiwemo Zanzibar) ni nchi ya kidemokrasia, CCM ndiyo iliyokubali kuanzisha upya mfumo wa vyama vingi baada ya Zanzibar kuvipiga marufuku muda mfupi baada ya mapinduzi mwaka 1964. Tushindane kwa sera na bila shaka watu watachagua chama kilichokuwa bora,’’ alifafanua Dk Shein.
Aliwaeleza wananchi kwamba yeye hivi sasa ni Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa sheria na katiba.
‘’Nitaitisha mkutano na waandishi wa habari na kuelezea kwa undani kilichokuwa kinaendelea katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Leo (jana) mwenzangu (Maalim Seif) aliwahutubia wandishi wa habari na kusema madai mengi sana. Nami nitafanya hivyo pia,’’ alisema.
Dk Shein aliwataka Wazanzibari kuimarisha amani na utulivu na kwamba Zanzibar na Tanzania ni kwa ajili ya wananchi wote, bila kujali rangi, dini na ukanda. Alisema kwamba watu wenye nia iliyojificha ya kuiharibu Zanzibar na Muungano hawatafanikiwa kamwe.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!