Tuesday, 12 January 2016
BENKI ZA BONGO ZIMEAJIRI MAJAMBAZI WASEMA POLISI ,MAMBO MAZITO YAFICHUKA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro.
Stori: Na Makongoro Oging’,
DAR ES SALAAM: Baadhi ya benki nchini zinadaiwa kuajiri baadhi ya wafanyakazi walio kwenye mtandao wa majambazi kutokana na wateja wengi kupigwa risasi na kufa wakitoka kuchukua pesa, uchunguzi wa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi Tanzania umebaini.
Hayo yalisemwa na baadhi ya askari hao wiki iliyopita walipozungumza na mwandishi wetu na kusema kwamba, waajiri wasipokuwa makini katika kuajiri watashangaa kuona wateja wao wanapigwa risasi na kuuawa kila kukicha.
“Haiwezekani kuwa wanaonyang’anywa fedha ni wale wanaotoka kuchukua benki kuliko wanaopeleka! Ina maana wezi wapo katika baadhi ya mabenki hivyo kunatakiwa kuwepo na umakini wakati wa kuwaajiri,” alisema askari mmoja kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar akiomba hifadhi ya jina lake kwa vile yeye si msemaji.
Afande huyo aliendelea kusema kuwa, baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu wa benki hizo wanapoona mteja anachukua fedha nyingi hufanya mawasiliano kwa njia ya simu kuwaeleza majambazi walio nje namna alivyovaa mteja huyo na kiasi cha fedha alichochukua.
Uchunguzi zaidi unaonesha kuwa, endapo hali hiyo haitadhibitiwa haraka huenda wananchi wakapatwa na hofu ya kuweka fedha zao benki kwa kuogopa kuporwa na kupigwa risasi wakienda kuzichukua.
Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita, lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro (pichani) ambapo alikiri kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi wenye mtandao na majambazi huku akisema jeshi lake limeweka mikakati kuhakikisha mtandao huo unasambaratishwa mara moja.
“Ni kweli kwamba, baadhi ya mabenki, si yote, yameajiri baadhi ya wafanyakazi, si wote wenye mtandao na majambazi. Kwa hiyo hata wao ni majambazi tu.
“Sasa tumejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kukamata pikipiki zinazohusika katika uhalifu. Pia tumeamua kuweka makachero nje na ndani ya mabenki, wapo polisi wa miguu, pikip iki na magari. Nina uhakika tutawadhibiti,” alisema Kamanda Sirro.
Aliendelea kusema kuwa, majambazi waliopo katika Kanda ya Dar es Salaam waanze kufunga virago kwani bila kufanya hivyo wajue watakamatwa wote na mtandao wao kumalizika. Pia aliwataka wamiliki wa mabenki kuwa makini wakati wa kuajiri wafanyakazi ili kuwapata wenye sifa njema na kuweka imani kwa wateja wao.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishina Suleiman Kova aliwahi kutamka kuwa, baadhi ya wafanyakazi wa ndani wa baadhi ya benki wana ushirikiano na majambazi. Akawatahadharisha wamiliki kuwa makini wakati wa kuajiri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment