Tuesday 12 January 2016

Yeyote atakayeguswa na kutaka kumsaidia awasiliane naye kwa namba ya simu 0768819621.

ugonjwa
Mashaka Andrea Malale akiwa na uvimbe mkononi mwake.
Stori: Deogratius Mongela
na Chande Abdallah, UWAZI
KAHAMA: Mashaka Andrea Malale (38), mkazi wa Kahama, Shinyanga anateseka kutokana na ugonjwa wa ajabu uliompata tangu akiwa mdogo na kusababisha alazwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili huku pia akidai kukimbiwa na mkewe aliyemtelekezea wototo wawili.

Mashaka ambaye amelazwa Sewa Haji, Wodi namba 23 hospitalini hapo, alisema kuwa ugonjwa huo wa ajabu alizaliwa nao kwa kupata alama nyeusi kwenye mkono wake kisha akapata uvimbe mdogo ambao kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, uvimbe huo nao ulizidi kukua na kufikia hali aliyonayo hivi sasa.
uwazi
Mashaka akionyesha uvimbe katika mkono wake na sehemu ya kifua.
AHANGAIKA HOSPITALINI
Akizungumza na waandishi wetu, Mashaka alisema kuwa mara baada ya uvimbe huo kukua sana alianza vipimo katika Hospitali ya Ushirombo iliyopo Bukombe, Geita na baadaye alihamishiwa Hospitali ya Bugando na kupelekwa Hospitali ya Nkinga, Tabora kabla ya Julai 27, 2015 kuhamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Kwa kifupi hali hii nimeishi nayo kwa miaka 38 kwa sababu nilizaliwa nayo, niliambiwa nimerithi kutoka kwa mama kwa sababu na yeye alikuwa na uvimbe mdogo mgongoni.
“Madaktari walisema kuwa ugonjwa huu unaitwa Fromabimitosis na unasambaa kwa njia ya damu ili kuupunguza natakiwa nifanyiwe operesheni na kwa muda wote huu natakiwa niwe nanunua dawa na kulipia kitanda na mimi sina hela kabisa.
MKE AMKIMBIA
“Tangu nilipoondoka kijijini kwetu na kuja huku, mke wangu naye ameondoka nyumbani na amewaacha watoto wangu mmoja ana miaka 17 na mwingine ana miaka 14, wote wapo kwa majirani na wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu naumwa sana. Niliambiwa tu ameondoka kutokana na huu ugonjwa wangu.
MAUMIVU MAKALI
“Nasikia maumivu makali kiunoni, kwenye mabega na kifuani kama unavyoona mfupa wangu hapa (akionesha kifuani chini ya uvimbe) ndiyo umehama kabisa na kushuka chini kutokana na uzito wa hizi nyama.
ALIA NA MSAADA
“Sina ndugu yeyote anayenipa msaada na wazazi wameshafariki, nawaomba sana Watanzania wanisaidie chochote niweze kutibiwa na kuwahudumia watoto wangu nao wasome.
“Ninasikia wenzangu wenye matatizo kama haya wanatibiwa huko India kwa shilingi milioni 5 sasa mimi sijui nitazitoa wapi, nawaomba sana watu wanisaidie niweze kupata tiba.
“Kama unavyoona hapa Muhimbili nimepunguzwa baadhi ya nyama na ninahitaji dawa nikizikosa tu, mkono unavimba na napata maumivu makubwa na kidonda hakikauki na nimeambiwa kinaweza kuoza,” alisema Mashaka kwa masikitiko.
Yeyote atakayeguswa na kutaka kumsaidia awasiliane naye kwa namba ya simu 0768819621.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!