Sunday 27 December 2015

LISHE DUNI,KAULI CHAFU BADO KAA LA MOTO KWA WAJAWAZITO


Historia ya tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa, moja ya changamoto inayowakabili wanawake wajawazito katika nchi zinazoendelea, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni kukosa lishe bora katika kipindi chote cha ujauzito.
 
Ni sababu ambayo mzizi wake umejikita katika pande nyingi; familia, elimu, tabia binafsi na mwenendo wa matabibu na uhalisia wa maisha.  
 
Kwa mujibu wa tafiti hizo, chanzo kikubwa kinachosababisha vifo vya kinamama wakati wa kujifungua, ni kupoteza damu nyingi.
 
Lishe bora kwa wajawazito, inaelezwa kuwa ndio kinga bora dhidi ya madhara yao, yakiwemo vifo. Sera ya serikali nchini, inaelekeza kwa kila mwanamke kujifungua, ni sharti aende kliniki na kupata ushauri sahihi kiafya.
 
Inaaminika kuwa, endapo mjamzito atahudhuria kikamilifu kliniki, itakuwa rahisi kwake kugundua usahihi wa afya yake, mahitaji ya lishe na yote hayo yanapofanyika kwa namna bora, ni wazi vifo kwa kinamama wajawazito vitapunguzwa na hatimaye kuzuilika.
 
CHANGAMOTO
Kwa bahati mbaya nchini, inaelezwa bado mwamko wa kinamama wa vijijini kwenda kliniki uko chini au katika hatua ya kufuata ushauri wa wauguzi na wakunga, kulinganisha na wenzao wa mijini. 
 
Tofauti ya kinamama wa mijini na mijini katika kutofuata ushauri, ni kwamba wa mijini hupuuza ushauri na wenzao wa vijijini kiwango chao cha uelewa kiko chini.
 
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Mwita Mwako, anasema wajawazito wengi hupuuza maelekezo na ushauri wanaopewa na wauguzi kuhusu lishe, hali inayoleta kasoro katika kiwango cha lishe na hatimaye wanakabiliwa na upungufu wa damu wakati wa kujifungua.
 
Dk. Mwako anasema, katika kipindi cha ujauzito, kinamama wanapaswa kuwa makini kutokana na changamoto za kiafya zinazowakabili, kama vile kukataa aina fulani ya vyakula na kutapika.
 
Mtaalamu huyo wa afya anasema kuwa, mama mja mzito anatakiwa kupewa maelekezo ya kukabiliana na hali hizo, ili kujijengea afya bora.
 
“Maelekezo wanayopewa na wauguzi, wanapaswa kuyafuata na kuzingatia, kwani wasipoyafuata, wanaharibu afya zao wenyewe na watoto na wakati mwingine, wanaweza kupoteza maisha,” anasema na kuendelea:
 
“Wakati wa kliniki, kinamama wote wajawazito hupewa elimu kuhusu lishe bora, hasa katika suala zima la kuhakikisha anakuwa na damu ya kutosha mwilini.
 
“Lakini cha kusikitisha, ni kwamba kinamama hao hupuuzia elimu hiyo, hali inayosababisha uwepo wa ongezeko la vifo vingi vitokanavyo na uzazi,” anasema Dk. Mwako na kutaja athari zinazoepukika na hilo, ni kupata kiharusi na kupoteza maisha
 
DHANA POTOFU
Rai nyingine anayotoa mganga mkuu huyo, ni kuepukana na mila potofu ya kutohudhuria kliniki na ni muhimu mjamzito kupata baadhi ya chanjo kabla hajajifungua.
 
Muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, Matilda Solomon, anawataka wajawazito wahudhurie kliniki ili wapate elimu ya bora ya kumlea mtoto awapo tumboni na mabadiliko yanayotokea katika kipindi cha miezi tisa cha ujauzito.
 
Anasema, ni wajibu wa kinamama wajawazito kuhakikisha wanahudhuria kliniki na kufuata ushauri wanaopewa na wataalamu wa afya, kuepuka vifo vitokanavyo na uzazi.
 
“Ili mama mjamzito awe na afya njema ya mwili na akili, ni lazima ale vyakula bora vyenye kumkuza mama kiakili na kimwili na mtoto pia,” anasema Muuguzi Matilda.
 
Mtaalamu huyo wa afya ya mjamzito, anaongeza kuwa katika kuhakikisha mjamzito anakuwa na afya bora, ni lazima ale vyakula vya kujenga na kulinda mwili, ili aepuke maradhi yanayoweza kumdhuru na aliyeko tumboni.
 
“Ili kuhakikisha mama anapata vitamini za kutosha, ni lazima apate mboga za majani na matunda kwa kiasi kikubwa na hii itasaidia kupunguza tatizo la kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua,” anasema.
 
LISHE MUHIMU
Matilda anataja vyakula vya kujenga mwili ni vya jamii ya protini, kama vile samaki, mayai, maharage, kunde, karanga, soya, mbaazi, kunde na maharage.
 
Ulinzi wa mwili kwa mjamzito ni jambo la lazima, kutokana na kukwepa magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza kumshambulia mama na mtoto aliye tumboni.
 
Matilda a anataja magonjwa hayo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ni kama vile ya njia ya hewa na mkojo, mafua, kikohozi, mkojo mchafu (UTI), maumivu ya tumbo, misuli, mifupa.
 
Anasema kuwa, yote yanaweza kutibiwa au kuzuiliwa kwa kula vyakula vya kulinda mwili, vyakula hivi pia husaidia kuongeza damu na kuzuia upungufu wa damu.
 
“Licha ya mama kupata lishe bora, pia anatakiwa kupata vitamini A,B,C,D,E, na K na kila moja ina kazi yake. Lakini, kazi kuu ni kulinda mwili, pia anatakiwa kupata madini ya aina tofauti kama chokaa au ‘calcium’, zink, madini ya chuma ‘potassium,’ ‘manganese,’ ‘chloride,’ sodium, magnesium, ambayo husaidia kuimarisha mwili na kuongeza damu,” anasema.
 
Anasema, upatikanaji wa madini na vitamini ndani ya mwili wa mwanamke mjamzito, kunaweza kumsaidia katika kushiriki katika shughuli nyingine za maendeleo.
 
WADAU WAKIRI
Baadhi ya wadau wanakiri upuuzaji maelekezo ya wauguzi na upungufu wa elimu kwa baadhi ya kinamama, hasa waishio vijijini, ni hali inayosababisha upungufu wa damu wakati wa kijifungua, kutokana na kuvuja damu nyingi wakati wa kujifungua.
 
Renalda Shao, mkazi wa Lekuruki wilayani Siha, anasema kuwa wakati wa kujifungua, kinamama wengi hupoteza maisha kutokana na upungufu wa damu.
 
Anasema, wengi wameathirika kutokana na kupuuza maagizo ya wauguzi na hilo liko zaidi vijijini, huku wakikosa uhimizwaji kutoka kwa waume zao.
 
Renalda anaioomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwashirikisha wanaume katika elimu ya afya ya uzazi, ili nao wafahamu matatizo yanayowakumba kinamama katika kipindi cha ujauzito.
 
“Licha ya kuwahimiza kinamama kwenda kliniki mara kwa mara na kuwalaumu kwa kutofuata maelekezo kwa ajili ya afya zao na watoto, pia hata kinababa wamekuwa kikwazo kikubwa,” anasema mdau mwingine – aitwaye Benadicta.
 
 “Matatizo mengi ya uzazi yanayotukumba sisi wanawake wengi, yanatokana na waume zetu kukosa elimu ya afya ya uzazi, ukizingatia ndiyo wasaidizi na washauri wetu wa karibu tuwapo majumbani,” anafafanua na kuongeza:
 
“Wanaume washiriki nasi kikamilifu kuwahudumia tuwapo majumbani kwa kutunguzia shughuli nzito pindi wanapogundua tu wajawazito na kuhimiza utumiaji wa vyakula vya kujenga mwili, ili kuepusha madhara makubwa ya uzazi.” 
 
KINAMAMA WANAOJIWEZA vs KAULI CHAFU 
uchunguzi ulioendeshwa na gazeti hili katika Kituo cha Afya cha Siha, Zahanati za Sanya Juu na Naibilie, Kituo cha Afya Magadini na Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro – Mawenzi, imegundua kinamama wengi wajawazito wenye, kipato hupuuza maelekezo ya wauguzi wakati wa kliniki.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!