Sunday 27 December 2015

MICHEZO: BUTLER ALICHAFUKA TOKA ZAMANI


MWAKA 1999, mwandishi wa kiuchunguzi maarufu, David Yallop alikuwa wa kwanza kubainisha kuhusu tuhuma za rushwa ambazo zilimtia doa Rais wa Fifa, Sepp Blatter. Mwandishi huyo aliandika ukweli kuhusu jinsi soka inavyoendeshwa.

Kitabu chake, “How They Stole the Game,” kilichochapishwa mwaka 1999, kilikuwa cha kwanza kubainisha ushahidi wa tuhuma za rushwa ambazo zilifanya watu wahoji ushindi wa Blatter katika urais wa Fifa mwaka 1998. Wiki moja baada ya Yallop kutoa kitabu hicho, aliyekuwa Rais wa Chama cha Soka cha Somalia, Farah Ado alidai hadharani kuwa alipewa Dola za Marekani 100,000 ili kumpigia kura Blatter.
Kutokana na hali hiyo, Blatter alikabiliwa na mzozo mkubwa katika Fifa na siku chache baadaye wale wanaompinga walipata nguvu baada ya Kamati ya Utendaji ya Fifa kushinda kura ya kuunda Kamati huru ya Ukaguzi ili kukagua menejimenti ya fedha za Fifa. Licha ya Yallop kutoa uchunguzi wake huo Machi 1999, Blatter mara zote amekanusha tuhuma hizo na kuwaeleza waandishi wa habari mwaka 1999 kwamba “Mchezo umeisha.
Filimbi imepulizwa. Wachezaji wamerudi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo”. Wakati huo, washirika wa Blatter walikanusha kuhusu tuhuma za hongo ili kupata kura na kumrithi Joao Havelange na kumshinda aliyekuwa Rais wa Uefa, Lennart Johannson. Inadaiwa kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Fifa kwenye Hoteli ya Meridien mjini Paris, Ufaransa walipewa bahasha za kaki saa chache kabla ya mkutano huo wa mwaka 1998.
Madai ya Fifa na washirika wake walidai kuwa walitoa malipo lakini yalikuwa malipo ya awali kwa vyama vya soka duniani ya Dola za Marekani 250,000 ambazo zilikuwa ni ruzuku kwa vyama maskini, na kudai hakukuwa na jambo lisilo la kawaida katika ugawaji wa fedha hizo rasmi za Fifa zitakazotumika kwa maendeleo ya soka.
Nakumbuka baada ya kutoka kwa kitabu hicho, gazeti la kwanza la michezo la kila siku nchini, Bingwa liliamua kukinakili kitabu hicho kwa nia ya kuwapa wasomaji wake ukweli kuhusu sakata hilo la Fifa ambapo inadaiwa kuwa Blatter alifadhiliwa fedha hizo na watu kutoka mojawapo ya nchi za Falme za Kiarabu. Haikushangaza wakati ule kuwa waliokuwa viongozi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), walijaribu kutaka gazeti hilo lisiendelee kunakili kitabu hicho na kuwapo kwa tishio la kulishitaki.
Hawakufanya hivyo na kitabu hicho chote kilichapishwa na Watanzania wapenda soka wakafahamu nini kilichojiri Paris mwaka 1998. Nimefanya rejeo hilo kwa makusudi hasa baada ya kile kilichotokea wiki hii baada ya Kamati ya Maadili ya Fifa kumfungia Kanali huyo wa zamani wa Uswisi miaka minane ya kutojihusisha na soka yeye pamoja na swahiba wake wa muda mrefu Michel Platini ambaye ni Rais wa Uefa.
Kwa waliobahatika kumsoma Yallop na yaliyotokea katika miaka 17 ya Blatter katika majengo ya Fifa pale Zurich, ni ushahidi tosha kuwa uongozi wake uligubikwa na rushwa ambayo alituhumiwa tangu siku ya kwanza anapata uongozi huo wa juu wa soka duniani.
Hivyo yanapotokea haya ya sasa ni dhahiri kuwa si mambo mageni kwa wapenzi wa soka waliokuwa wakifuatilia soka la kimataifa kwa miaka kadhaa sasa kwani wameshuhudia Fifa ikikumbwa na kashfa nzito za rushwa chini ya Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Fifa ambaye aliingia katika shirikisho hilo tangu mwaka 1975.
Ilianza misukosuko kati ya washirika wa masoko wa Fifa, ISL ambayo ilidaiwa kuwa iliwahonga baadhi ya maofisa wa Fifa. Shirika la Ujasusi la Marekani, FBI lilianzisha uchunguzi dhidi ya Blatter, aliyekuwa mtangulizi wake, Joao Havelange na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Fifa, Ricardo Teixeira ambao wanadaiwa kuhongwa Dola za Marekani milioni 100 ili kampuni hiyo ipate haki za matangazo ya biashara katika miaka ya 1990.
Lakini pia wakati wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Fifa mwaka huu ambao Blatter alishinda, maofisa wake kadhaa walitiwa ndani wakichunguzwa na FBI kwa kutokana na madai ya rushwa katika kandarasi mbalimbali zikiwamo za kutoa uenyeji wa Kombe la Dunia zikihusishwa nchi za Afrika Kusini, Qatar na Urusi.
Ndiyo maana haikushangaza kuwa Kamati ya Maadili ya Fifa ambayo ni kamati huru, kumsimamisha Blatter na Platini aliyekuwa na ndoto za kuwania urais wa Fifa, siku 90 kabla ya wiki hii kuwahukumu kifungo cha miaka minane kutojihusisha tena na soka, mchezo unaopendwa na wengi duniani.
Maswahiba hao wamefungiwa baada ya uchunguzi huo wa Kamati ya Maadili kuwatia hatiani na rushwa ya kupokea na kutoa malipo yanayokadiriwa kufikia Pauni milioni 1.3 za ‘malipo hewa’ yaliyofanywa na Fifa yakiidhinishwa na Blatter kwenda kwa Platini mwaka 2011.
Ni ukweli usiofichika kwamba mtu ambaye anatuhumiwa kupata uongozi au nafasi kwa rushwa, hawezi kuwa kinara wa kupambana na uovu huo, na hali hii inajidhihirisha wakati wote wa uongozi wa Blatter ambao umeshuhudia shirikisho hilo likigubikwa na rushwa kila kona.
Blatter kama ambavyo baadhi ya watu wanataka dunia iamini, kuwa alivisaidia vyama vidogo au masikini vya soka duniani hasa vya Afrika na Asia, lakini hawezi kukwepa tuhuma hizi za rushwa kwamba chini ya uongozi wake, Fifa imegeuka kuwa genge la wala rushwa na jina lake lilipoteza sifa miongoni mwa wapenzi wa soka.
Kwa mujibu wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga ambaye mwaka 1998 alipiga kura kuchagua Rais wa Fifa jijini Paris, kosa la rushwa linatakiwa kifungo cha maisha kama Blatter alivyowahi kumfungia Mohamed bin Hammam wa Qatar, kwa madai ya rushwa ya tenda ya kuandaa Kombe la Dunia, hivyo na yeye alistahili kufungiwa maisha.
Si hilo tu, Ndolanga aliwataka wajumbe wanaowakilisha vyama vya soka vya Bara la Afrika katika Fifa wawe wanazungumza kwenye mikutano na vikao mbalimbali ili kuondoa dhana ambayo ilikuwa imejengeka kuwa Blatter anasaidia Afrika wakati pesa inayotumika ni ya Fifa na inapitishwa na vikao husika na siyo hisani yake.
Afrika na Asia ‘watammiss’ Blatter kama mmoja wa viongozi wa soka duniani walionesha dhamira ya dhati kusaidia mabara haya katika kuendelea kisoka, lakini kwa ujumla uongozi wake uligubikwa na rushwa ambayo mahali popote pale ni saratani inayopaswa kuondolewa inapoingia.
Kama alivyoeleza mwenyewe mwaka 1999, mchezo umeisha na filimbi imepulizwa, ni wakati wa mabadiliko katika soka. Blatter kama alivyoona dalili na kueleza kuwa angejiuzulu Februari mwakani, anapaswa kukaa pembeni ili mtu mwingine aje asimamie mabadiliko ya kweli ndani ya Fifa na kurejea hadhi yake. Pole Blatter na kwa heri.fica, Roma, Olympiakos, Porto au Gent.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!