Sunday, 27 December 2015

MIL 20 ZA KOVA HAZINA MWENYEWE




Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Sulemain Kova, ameitaka tena jamii kuchangamkia zawadi ya Sh. milioni 20 alizoahidi kutoa kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Regional Cargo Services, Abdulkarid Abdi.



Abdi anatajwa kufanikisha mpango wa kutolewa kwa makontena 329 kutoka bandari kavu (ICD) ya Azam bila kulipiwa kodi.

Kamanda Kova aliyasema hayo jana jijini katika mahojiano na Nipashe, na kuongeza kuwa hadi sasa bado wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo.

Aliwaomba wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi ili Abdi afikishwe mikononi mwa polisi. Polisi haijatoa picha yake ili kurahisisha utambuaji huo, hata hivyo.

Aidha, Kova alisema Abdi ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni za Jas Express Freight na Ex Clearing and Forwarding Co ambazo zilitumika kutoa makontena hayo.

Baada ya sakata la makontena kuibuliwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwezi uliopita, mtuhumiwa alianza kutafutwa na kila alipopigiwa simu ya mkononi ilikuwa inaita bila kupokelewa.

Aidha, Jeshi la Polisi lilimtaka mtuhumiwa huyo kujisalimisha kwa hiari yake mwenyewe badala ya kusubiria akamatwe lakini mwezi mmoja baadaye ameendelea ‘kula kuku’ uraiani.

Wakati huo huo, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Sulemain Kova aliwahi kusema kuwa walikuwa wanawashikiliwa watuhumiwa wawili akiwamo Mkurugenzi wa Kampuni ya Jas Express na Afisa Forodha wa kampuni hiyo, Godfrey Masilamba.

Watuhumiwa hao walihojiwa kwa tuhuma za kufanikisha ukwepaji wa kodi ulioisababishia serikali hasara ya mabilioni.

Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais, John Magufuli, ilibaini ubadhirifu na ukwepaji kodi wa makontena 329 ambayo yameisababishia serikali hasara ya zaidi ya Shilingi bilioni 80.

Kufuatia sakata hilo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), Rished Bade, alisimamishwa kazi huku polisi ikiwashikilia na maofisa kadhaa waandamizi wa mamlaka hiyo kwa uchunguzi na wengine akiwamo Kamishina wa Forodha, Tiagi Masamaki, kufikishwa mahakamani.

Wafanyabiashara waliokwepa kodi kwenye sakata hilo walipewa siku saba na Rais Magufuli walipe kwa hiyari yao kodi wanazodaiwa na tayari baadhi yao walijitokeza na kulipa Sh. bilioni 11.4.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!