Saturday 7 November 2015

MACHINJIO YA VINGUNGUTI NI HATARI


Wakati kiasi cha nyama ya ng’ombe tani 120, sawa sawa na ng’ombe 1,200 kinaliwa jijini Dar es Salaam kila siku, machinjio yanayotegemewa yaliyopo Vingunguti manispaa ya Ilala, yamekithiri kwa uchafu, Nipashe limegundua.

Pamoja na uchafu unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ubovu wa miundombinu yake, nyama inabebwa kichwani pasipo kuwapo kifaa cha kuzuia isigusane na nywele. 
Wabebaji wengine wanaiweka nyama kwenye mabega ama mgongoni wakiwa hawajavaa vazi maalum, lakini zaidi wakitokwa jasho ‘linaloishia’ kwenye nyama.
Nipashe imeshuhudia nyama ikibebwa katika mazingira hayo hatarishi kwa afya ya mtumiaji, wakati nyama ikitolewa eneo la uchunaji ngozi kupelekwa mahali pa kupima uzito, kucharangwa ama kupakiwa kwenye vyombo vya usafiri.
Miongoni mwa wanaobeba nyama kwenye machinjio hayo wanafuga nywele ndefu wakati wanaobeba mgongoni wanakuwa wamevaa mavazi machafu yasiyostahili kugusana na nyama iliyo kitoweo cha walaji nchini.
Ubebabaji wa nyama kichwani unasababisha wahusika (wabebaji) kutapakaa damu vichwani mwao, inayogandamana na nyama ambayo mwisho wa siku inamfikia mlaji. Hali hiyo ipo kwa wanaobeba nyama begani ama mgongoni wakiwa wamevaa nguo zisizokuwa katika ubora unaokubalika kwa mujibu wa misingi na kanuni za afya.
Katika hali inayostaabisha ubebaji wa aina hiyo unafanyika mbele ya macho ya wataalamu wa afya wanaokuwapo kwenye eneo hilo wakisimamia na kutekeleza majukumu yao. Nipashe ilimtafuta msemaji kuhusu suala hilo, Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi, Manispaa ya Ilala, Dk. Audifas Sarimbo, alisema kuna sare zimewekwa kwa  wafanyakazi wote wanaobeba nyama, na kwamba wale wanaokiuka utaratibu watachukuliwa hatua kwa kuwa kufanya hivyo kunahatarisha usalama wa nyama. Alisema kuanzia wiki ijayo watawaondoa watu wote wanaofanya biashara nje ya jengo hilo. 
NARCO YAKEMEA
Meneja Mkuu wa Narco, Dk. John Mbogoma anakemea hali hiyo akisema ubebaji nyama unahitaji mazingira safi na usalama, vinginevyo kitoweo hicho kitasababisha madhara ya afya kwa watumiaji wake.
MAENEO YA KUCHARANGA
Nipashe haikuishia hapo bali ilifuatilia kubaini mahali zinapopelekwa nyama hizo, ikafika kwenye eneo linatumika kwa kuzicharanga ambalo hata hivyo ni chafu lisilostahili kutumika kwa shughuli hiyo.
Ni eneo lisilokuwa na sakafu badala yake nyama inawekwa na kucharangwa kwa kutumia shoka ikiwa kwenye gogo. 
Kiasi cha nyama kinapokuwa kikubwa, inatandikwa mifuko ya plastiki  chini ikitumika kwa ‘kulundika’ bidhaa hiyo ikisubiri kucharangwa.
WIZI
Kukosekana kwa umakini kwa mmiliki wa nyama kumekuwa kukitoa mwanya wa wizi katika hatua tofauti hasa ya kucharanga.
“Endapo mhusika hatasimamia nyama yake wakati inacharangwa, kuna uwezekano mkubwa wa kuibiwa,” anasema mmoja wa wafanyabiashara aliyejitambulisha kwa jina moja la Neema.
Licha ya mazingira kuwa machafu, eneo linalotumika kwa kucharanga nyama ni finyu lisilochochea ufanisi kwa wafanyakazi wa machinjio ama wateja.
Ufinyu wa eneo hilo unasababisha msongamano wa watu wanaoingia wakiwa wamevaa viatu wakikanyanga maeneo yanayotumika kwa kuhifadhi nyama.
Hali kama hiyo ipo kwenye eneo la machinjio ambalo limetapakaa damu kiasi cha ‘kuenea’ kwenye viatu vya kila anayeingia humo.
MIFEREJI
Mchakato wa kuchuna mfugo uliochinjwa unahitaji matumizi ya maji yanayosafiri kwenye mifereji isiyotuama maji.
Lakini kwenye eneo hilo, mifereji mingi imeziba hivyo kusababisha maji yaliyochanganyika na damu kutuama, hali inayotishia magonjwa ya mlipuko  na harufu katika eneo hilo. James Charles ni mnunuzi wa nyama kwenye machinjio hayo, anathibitisha kuwa mazingira yaliyopo si rafiki kwa afya za wadau wakiwamo wachinjaji, watoa huduma na wanunuzi.
Anasema kutokana na hali hiyo, ipo haja kwa serikali kuweka mkakati madhubuti utakaosababisha kudhibiti udhaifu uliopo kwenye miundombinu ya machinjio hayo ili ikidhi vigezo, misingi na kanuni za afya.
MNADANI HALI TETE
Kama ilivyo kwa machinjio ya Vingunguti, eneo la mnada wa ng’ombe huko Ruvu linalotumika kwa kuhifadhi na kuuza mifugo hiyo, linakabiliwa na miundombinu mibovu licha ya tozo za ushuru zinazokusanywa kutoka kwa wafanyabiashara.
WASAFIRISHAJI
Pamoja na nyama inayochinjwa kuwa kwenye mazingira machafu, lakini usafirishaji wa ng’ombe kutoka mikoa mbalimbali unachangia kuidhoofisha nyama baada ya kuchinjwa. Miongoni mwa vyanzo vinavyochangia hali hiyo ni ukosefu wa malisho na maji kwa mifugo inayosafirishwa kati ya siku tatu hadi tano kwa kutumia magari, bila kula wala kunywa. Mmoja  wa wasafirishaji wa ngombe, Omary Kalimba, anathibitisha hali hiyo na kuongeza kuwa msongamano wa ng’ombe wengi kwenye gari unachangia pia kuathiri afya na ubora wa nyama. “Mara nyingi tunaposafirisha idadi kubwa kwenye lori, ng’ombe wanasumbuka kwa msongamano na inapotokea wengine kuanguka hasa kutokana na dereva kushika breki za ghafla, wanaweza kukanyagwa hadi kufa,” anasema.
MACHINJIO YA RUVU
Nipashe ilifika katika eneo  la Ruvu wilayani Bagamoyo palipo na mradi wa machinjio ya kisasa uliopangwa kugharimu Shilingi bilioni tisa. Hata hivyo mradi huo ulisitishwa mwaka juzi kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo, Suma JKT kukiuka makubaliano ya mkataba.
Mradi huo ulitarajiwa kuwezesha kuchinja ng’ombe 1,000, mbuzi 1,500 huku ukitoa ajira zaidi ya 200. Kushindwa kukamilika kwa mradi huo kumesababishia kuanzishwa kwa machinjio ya mbuzi ambayo yapo eneo Mazizini, njia ya kwenda Kitonga huku Ruvu wakiendelea wakichinja kwa njia za kiasili na kuning’iniza nyama juu ya miti. Kwa hivi sasa eneo la mradi huo halina miundombinu zaidi ya kamba zilizotundikwa kwenye miti, zikitumiwa na wachinjaji wa mbuzi kwa njia za asili wanalipia ushuru wa Sh 500 kwa kila mbuzi anayechinjwa.
Pia eneo hilo ambalo lipo umbali wa takribani mita 570 kutoka barabara kuu ya Dar es Salaam kwenda Morogoro ni chafu kutokana na kutofanyiwa usafi baada ya kuchinja.
Nipashe ilielezwa na vyanzo tofauti kuwa kutokana na eneo hilo kuwa mbali na barabara, wachinjaji wanalazimika kubeba maji lita 10 za ujazo kwa ajili  kuoshea  nyama na utumbo lakini hayatoshi. 
Baadhi ya wenyeji wa eneo hilo wanaelezea kuishi katika mazingira magumu huku serikali ikiacha kuchukua hatua.
 “Sisi tukizungumzia jambo hili tunapewa vitisho, hivyo hii hali tumeizoea, mvua ikinyesha hata kula tunashindwa na huu uchafu wote unaouona unaenea hadi kwenye mto Ruvu,” anasema mkazi wa Ruvu anayeomba jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ruvu,  Kambona Kwalo, anasema hakuna haja kwa wakazi hao kuilalamikia hali hiyo kwa vile eneo hilo lilitengwa mahususi kwa ajili ya machinjio. Kwalo anasema mpango wa serikali wa kujenga machinjio hayo bado upo na kwamba wanavijiji wanapata taarifa za mchakato wake kupitia vikao vyao.
Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco)  inachinja ng’ombe kati ya watatu hadi watano kwa siku na kuuza nyama kwa wananchi, lakini hawana machinjio ya kisasa.
Machinjio yaliyopo Narco yaliezuliwa mabati kutokana na upepo mkali uliowahi kutokea kwenye eneo hilo, hivyo kuwalazimu kujenga ya muda.
Meneja Mkuu wa Narco, Dk. John Mbogoma, anasema sekta ya nyama inahitaji uimarishaji wa miundombinu, kuwapo kwa viwanda na mazingira mazuri ya biashara.
Anasema serikali ilibuni mradi wa Ruvu kuwa machinjio ya kisasa lakini Suma JKT hawakufanya vizuri hivyo kusitishiwa mkataba wao. Hali hiyo ilifikia baada ya majadiliano ya muda mrefu ikiwamo shauri lilihitimishwa kwa Suma JKT kuamriwa kulipa Sh. milioni 800 kutokana na kusitishiwa mkataba huo. Dk. Mbogoma anasema kwa sasa wapo katika mchakato wa kumpata mzabuni mwingine ili kuendeleza mradi huo na tayari kampuni kadhaa za ndani zimeomba zabuni hiyo. “Tunaendelea na mazungumzo na ifikapo Desemba tunatarajia kuwa ujenzi utaanza,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk. Mbogoma, mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 20 (sawa na takribani Sh  bilioni 42).
Anasema mradi wa Ruvu ukikamilika, machinjio ya Vingunguti yatageuzwa kuwa kituo cha usambazaji nyama zinazotokea eneo la mradi (Ruvu).
NYAMA TANI 120 ZATAFUNWA DAR
Dk. Mbogoma anasema takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa nyama yenye uzito wa tani 120 za nyama (sawa ng’ombe 1,200) inaliwa jijini Dar es Salaam kila siku, hivyo kuwa moja ya sababu ya kutoa kipaumbele kwa sekta hiyo.
Kwa mujibu wa Dk. Mbogoma, kama kutakuwa na mikakati mzuri kwa sekta hiyo, uzalishaji wake utaongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi kwa kiwango kikubwa.
Anasema licha ya kuchinja mifugo, Tanzania inasafirisha kiasi cha ng’ombe 300,000 kwenda Kenya ambao baada ya kuchinjwa, nyama inarejeshwa nchini na kuuzwa kwenye maduka makubwa maarufu kama Super markets.

NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!