Tuesday, 25 August 2015

MFADHILI MKUU WA MATUKIO YA MASHAMBULIZI AGUNDULIKA

Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
 

Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
 

IMEBUMBULUKA! Hatimaye Jeshi la Polisi Tanzania (PT) limeanika picha ya mtu anayedaiwa kuwa ndiye mfadhili mkuu wa matukio mbalimbali 


yanayohusishwa na ugaidi likiwemo lile la mauaji ya watu saba kwenye Kituo cha Polisi Stakishari, Dar lililotokea saa 5 usiku, Julai 12, mwaka huu na yale mapigano ya Amboni, Tanga.
 

Mtu huyo aliyetambulika kwa jina la Ally Mtozen Hery ambaye anadaiwa kuishi kwa kujibadili kama kinyonga kwa muonekano wa sura, wakati mwingine huvaa mavazi ya kike ili asijulikane kirahisi.
 

Akizungumza na Uwazi juzikati, Kamishna wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema uchunguzi uliyofanywa na kikosi kazi cha jeshi hilo umebaini kuwa, mtuhumiwa huyo ana mtandao mpana na ndiye mfadhali mkuu wa matukio mbalimbali ya uvamizi, mashambulio na uporaji wa silaha yanayotokea nchini.

Suleiman Kova akionyesha picha ya mtuhumiwa huyo.
 

Kova aliongeza kuwa, hivi karibunim Hery amehusika katika kufadhili tukio la Amboni Tanga, Mkuranga, Stakishari na mengineyo lakini hatimaye jeshi la polisi kwa kutumia kikosi cha intelijensia kimeweza kubaini nyendo zake na kuinasa picha yake hiyo.
 

“Tunachotaka mtu huyo ajitokeze mara moja na kujisalimisha polisi. Kwani hata afanyaje lazima tutamkamata tu,” alisema Kamishna Kova.
Akaongeza: “Ile milioni 50,000,000 iliyotangazwa na IGP Ernest Mangu sasa imefikia mahala pake kwa mtu atakayeweza kusaidia kupatikana kwa mtuhumiwa huyo.”
 

Kova aliendelea kusema mtuhumiwa huyo wakati mwingine hupenda kutembelea Pemba, Tanga, Dar na ukanda mzima wa Pwani.Katika mahojiano na Kamishna Kova alisema hadi sasa, watuhumiwa tisa wanashikiliwa na jeshi hilo kutokana na tukio la Stakishari.
“Si vyema kuwataja kwa majina tunaowashikilia kwa sababu za kiupelelezi lakini hadi sasa kwa jitihada za jeshi letu makini tunawashikilia watuhumiwa tisa na mahojiano yanaendelea,” alisema Kova.
 

Mbali na mtuhumiwa huyo kusakwa na jeshi la polisi, mtuhumiwa mwingine aliyekuwa akisakwa na jeshi hilo amejisalimisha polisi akiwa na wake zake wawili na sasa anahojiwa kwa kina.
 

Aliongeza kusema mtuhumiwa huyo aliyejisalimisha polisi aliwahi kuwa mtumishi ndani ya jeshi la polisi lakini alifukuzwa kazi mwaka 1998 kutokana na kutoeleweka kwa nyendo zake.
 

Polisi huyo aliyeachishwa kazi akiwa na cheo cha sajenti anafahamika kwa jina maarufu la Mzee Mzima ambapo akiwa kazini kitengo cha redio (999) ambacho hushughulikia matukio ya uhalifu kwa haraka nyendo zake zilikuwa hazieleweki ndani ya jeshi hilo.
 

“Hatuwezi kuvumilia damu za askari wetu zikipotea bure. Ni lazima tuhakikishe kazi tunaifanya ipasavyo na hao watuhumiwa tisa tunaowashikilia wanaendelea kutupa taarifa muhimu,” alisema Kova

CHANZO:GPL

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!