KONDAKTA wa daladala hii hakufahamu kama angekutwa na haya masahibu. Hakujua kama mdomo wake ungemponza na kujikuta katika majanga makubwa ya kupoteza macho. Hakujua kwamba katika daladala wamo watu wenye tabia na hulka tofauti.
Hakutaka kuamini ukweli kwamba, katika usafiri huo wa umma, upo uwezekano wa kuwamo ‘wanga’ vibaka, majambazi na wacha Mungu. Laiti angelijua haya, kondakta huyu asingezozana na abiria huyo. Tatizo alimchukulia kwa mtazamo wa kawaida wa ‘kikondakta’ kama ilivyo kwa makondakta wengi dhidi ya abiria. Angejua kwamba mtu anayezozana naye si abiria wa kawaida, bali ni mtu asiye na huruma wala utu, huyo kondakta angekubali yaishe.
Ngoja sasa niwamegee juu ya kisa hiki. Ingawa jicho langu halikushuhudia moja kwa moja kisa hiki, lilipata fursa ya kukutana na mashuhuda. Walisimulia kilichomkuta kondakta na abiria waliokuwa kwenye daladala moja inayofanya safari zake kati ya Mbezi na Posta. Mashuhuda hawa wakaeleza kilichojiri baada ya gari hilo kufika kituo cha Kimara. Wakasema, kondakta na abiria katika daladala hiyo, walianza kuzozana kwa kujibizana.
Haijulikani chanzo ilikuwa ni nini. Lakini kama ilivyo kawaida katika daladala, mzozo mwingi huanzia ama kwenye kudai nauli au kusogeza abiria wabanane aweze kupakia wengine. Siyo jambo la ajabu, kushuhudia makondakta walio wengi wakitoa kauli za kero kwa abiria. Au wakati mwingine, kushuhudia abiria akimjibu kondakta vibaya licha ya kuambiwa kwa ustaarabu. Wapo abiria wengine ni wakorofi na wababe hivyo wakikutana na makondakta wenye kero, lazima pachimbike.
Ndivyo ilivyojitokeza kwenye daladala hiyo. Inadaiwa baada ya kujibizana, huku kondakta akimdhihaki abiria huyo kwamba hana cha kumfanya, (abiria) naye alimhadharisha kondakta kwamba atamfanyia kitu ambacho hatakisahau maishani. Katika mwendelezo wa kuzozana, inadaiwa abiria huyo alichomoa chupa ndogo iliyosadikiwa kuwa na kimiminika, akammwagia kondakta machoni. Mashuhuda wanasema walishuhudia kondakta akihaha kutokana na macho kuathirika.
Wakati abiria huyo akishuka haraka kutoka kwenye daladala, kondakta alipiga kelele za ‘mwizi’. Inadaiwa watu waliokuwa karibu kituoni hapo, walimshambulia huyo abiria na kumpa kipigo cha mbwa mwizi. Haijulikani kilichoendelea baada ya hapo. Hata mimi sifahamu kama macho ya kondakta yameona tena. Wala sifahamu kama abiria huyo amepona baada ya kipigo kutoka kwa watu wenye hasira. Kwa ujumla haya ndiyo majanga ndani ya usafiri wa daladala.
Kwa kuzingatia majanga haya, nina kila sababu ya kukaribisha kwa mikono miwili mabasi maalumu yatakayotoa huduma chini ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT). Uwezekano wa kupumua na vioja vya daladala ni mkubwa kutokana na sifa zilizotolewa kuhusu mabasi hayo. Idadi ya mabasi yanayotarajiwa kutoa huduma chini ya mradi, ni 76. Tayari mabasi mawili yameshaingizwa nchini na yanatumika kufunza baadhi ya madereva uendeshaji wake.
Mabasi hayo yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 100 na 190 kwa mara moja, ujio wake na kuanza kwa huduma za BRT, ndiyo mwisho wa daladala za kawaida kati ya Kimara na Kivukoni, katika Barabara ya Morogoro. Mabasi hayo yanayotarajiwa kutumia dakika 20 kutoka Kimara hadi Kivukoni, ndani yana viti kwa ajili ya wazee, wajawazito na wenye ulemavu. Pia yana mikanda maalumu kwa ajili ya abiria wanaosimama.
Vituo vitakuwa na ulinzi kuhakikisha hakuna shughuli yoyote itakayoendeshwa zaidi ya kuwapo abiria pekee. Kikubwa zaidi, ni kwamba, mabasi hayo hayatakuwa na makondakta wala wapiga debe kutokana na mfumo wake wa kisasa wa ukusanyaji nauli. Hakutakuwapo tena mfumo wa makondakta kukusanya fedha. Badala yake, ukataji tiketi utakuwa ni wa kisasa; wa kielektroniki ambao utaratibiwa chini ya mfumo maalumu.
Aidha, mamlaka zinazohusika na huduma hiyo, zinasema wanaangalia uwezekano wa kuhakikisha hakuna mwingiliano kati ya dereva na abiria. Ina maana kazi ya dereva itakuwa ni moja tu; kusafirisha abiria kwa ustaarabu na kuwafikisha waendako. Sifa nyingine zinazoainishwa ni kwamba, madereva wa mabasi hayo wanatarajiwa kuwa waliofuzu mafunzo. Pia wanatarajiwa kuwa wastaarabu kuanzia mavazi hadi kauli zao.
Kama hayo yaliyoelezwa na mamlaka yatatekelezwa ipasavyo, ni dhahiri vituko, visa mkasa, kero na karaha za daladala katika njia hiyo ya Barabara ya Morogoro, vitakoma. Hatimaye, usafiri huo wa umma utageuka kuwa tegemeo kwa watu wote wakiwamo wanaolazimika kuingia gharama kubwa kutumia magari binafsi, kuepuka kero za daladala. Sasa yametimia. Tukaribishe mabasi haya kwa mikono miwili na tutakie kila la kheri mradi huo ili hatimaye, tupumue na vioja vya daladala.
No comments:
Post a Comment