Kilo 262 za pembe za ndovu zilizokuwa zinasafirishwa kutoka Dar es Salaam kwenda Beijing, China zinadaiwa kukamatwa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zurich, Uswisi zikiwa kwenye mabegi nane, mamlaka ya Forodha ya Uswisi imeeleza.
Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema imeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Pembe hizo zinazokadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 412,000 sawa na Sh. milioni 873.4 zilikamatwa zikiwa zinasafirishwa na raia watatu wa China, waliokuwa wanasafiri kutoka uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam kwenda Beijing nchini China kupitia Zurich.
Mkuu wa Idara ya Forodha kwenye viwanja vya ndege nchini Uswisi, Heinz Widmer, alisema jana kuwa inakadiriwa meno hayo yanatokana na kuuawa kwa tembo 40 hadi 50.
Taarifa zinaeleza kuwa mbali ya pembe za ndovu, raia hao walikamatwa wakiwa na kilo moja ya meno na kucha za simba.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa raia hao walikamatwa kwenye msako wa kushtukiza uwanjani hapo Julai 6, mwaka huu uliofanywa na maofisa wa forodha wa Uswisi.
“Meno hayo ya tembo yaligundulika yakiwa yamekatwa katwa vipande 172 na kuhifadhiwa kwenye mabegi nane yaliyokuwa yamebebwa na raia watatu wa China ambao walikuwa wanasafiri kutoka Dar es Salaam Tanzania kwenda Beijing,” alieleza Widmer.
Aidha, alisema Wachina hao walikamatwa na meno 21 ya simba na kucha 35 za simba ambazo bado thamani yake haijajulikana.
Kufuatia taarifa hizo, Serikali ya Tanzania imesema inafuatilia kwa kina kubainui ukweli.
Taarifa ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kwa vyombo vya habari jana ilieleza kuwa Wizara inafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) na vyombo vya ulinzi na usalama.
Aidha, alisema watakaobainika kuhusika kwenye ujangili huo watachukuliwa hatua za kisheria.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Interpol nchini, SACP Gustavus Babile, aliiambia NIPASHE jana kuwa: “Jana (juzi), niliwasiliana na mamlaka za Uswisi, lakini hadi jioni hawakuwa wamenipa majibu na sasa nipo safarini kuelekea Dodoma, sijapita ofisini kujua kama wamejibu nini.”
Takwimu zinaonyesha kuwa majangili huua tembo 35,000 kila mwaka nchini.
No comments:
Post a Comment