Sunday, 26 July 2015

WAGOMBEA ADC WAONYA WAUZA UNGA

Mwanachama wa ADC anayewania kuteuliwa na chama
Wanachama watatu wa Alliance for Democratic Change (ADC) wamechukua fomu za kuwania urais kupitia chama hicho, huku wakiahidi kukomesha mauaji ya albino na biashara ya dawa za kulevya.

Waliochukua fomu jana ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara Ndogondogo, Abubakary Rakesh, mjasiriamali Chief Yemba na mwanafunzi wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Emmanuel Maganga.
Wanachama hao walikabidhiwa fomu hizo jana na Naibu Katibu Mkuu wa ADC, Doyo Hassan Doyo mbele ya mlezi wa chama hicho, Hamad Rashid Mohamed.
Wanachama hao walikabidhiwa fomu hizo katika hafla iliyohudhuriwa na wanachama na wafuasi wa chama hicho baada ya kulipa Sh500,000 kama gharama ya fomu ya kugombea urais.
Akizungumzia mikakati yake, Rakesh ambaye ni mlemavu wa miguu alitangaza vita kwa wauaji wa albino na wauzaji wa dawa za kulevya.
Alisema akichaguliwa kuwa rais mtu yeyote atakayethibitika mahakamani kuwa ameua albino naye atauawa.
Alisema atapambana na rushwa na kwamba atashawishi watakaopatikana na rushwa kufungwa miaka 50 jela ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema anawania nafasi hiyo kwa sababu waliokuwa wakiwania nafasi ya urais kupitia CCM hawajawahi kuzungumzia kundi la walemavu na wafanyabiashara ndogo ndogo.
Alisema, yeye akiwa rais atahakikisha mtu yeyote anayemwoa mwanamke mwenye ulemavu na mwanamke atakayeolewa na mwenye ulemavu wataondolewa kodi.
“Nitavipunguzia kodi viwanda vitakavyoajiri idadi ya walemavu itakayopangwa ili kuwaongezea ajira kwa kundi hilo,” alisema.
Akizungumzia ulemavu wake wa miguu, alisema, anaweza kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi kwa sababu Ikulu si sehemu ya kubeba magunia.
Akizungumza, Yemba alitaja vipaumbele vinne ambavyo anaamini vitawaondolea matatizo Watanzania ikiwamo kuboresha huduma za afya.
Alisema atahakikisha kila Mtanzania anakuwa na afya bora ili aweze kufanyakazi kwa ufanisi.
Yemba alisema kipaumbele cha pili kitakuwa maji kwa kuwa tatizo hilo limekuwa likiwatesa Watanzania kwa muda mrefu.
Alisema Serikali haina nia ya dhati kukabiliana na tatizo hilo ndiyo maana bajeti za maji hazitengewi fedha za kutosha.
Mwanafunzi wa OUT, Emmanuel Maganga alisema akichaguliwa kuwa rais, atahakikisha anawaongezea walimu mishahara.
ili kukuza elimu.
Maganga anayesomea kozi ya ukufunzi wa walimu, alisema kushuka kwa kiwango cha elimu nchini kunatokana na kupuuza masilahi ya walimu.
“Kama kuna kitu kimekosewa ni Serikali kupuuza masilahi ya walimu nikichaguliwa kazi ya ualimu nitaifanya kuwa na hadhi ili kila mtu aipende,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!