Sunday, 26 July 2015

JAMBAZI LAKAMATWA LIKIJIANDAA KUVAMIA KITUO CHA MAFUTA


PICHA HAIHUSIANI NA HABARI HII
Jeshi la Polisi mkoani Pwani  linamshikilia Hassan Justine maarufu kwa jina la Mbwambo (23), mkazi wa Kigogo Freshi  jijini Dar es Salaam, baada ya kukutwa na silaha aina ya shotgun akitaka kuvamia kituo cha mafuta cha Camel kilichopo katika Kata ya Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mjini.



Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Jafary Ibrahimu, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa  Julai 12, mwaka huu wakati akijiandaa kufanya uhalifu huo ambapo kabla ya kutimiza adhima yake alitiwa nguvuni na askari wa jeshi hilo.

Kamanda Ibrahimu, alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya kunasa katika mtego uliowekwa na jeshi hilo katika eneo husika  kufuatia taarifa zilizotolewa na raia wema waliokuwepo katika kituo hicho.

Alisema, mtuhumiwa alikuwa na wenzake ambao hawakujulikana idadi yao lakini walifanikiwa kutoroka na kutokomea. 

Aidha, Ibrahimu alisema kuwa baada ya kuhojiwa kwa mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na matukio mengine  ya uporaji  kwenye kituo cha mafuta cha Mogas kilichopo eneo la Mwendapole wilayani Kibaha pamoja na Mkata wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Katika tukio lingine, jeshi hilo limekamata silaha mbali mbali katika operesheni iliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo moja ya silaha hizo ni bunduki aina ya SMG yenye namba 14302621.

Mbali na bunduki hiyo zilikamatwa risasi  30 za SMG ndani ya magazine, visu 11, mapanga manne, majambia matatu, risasi 103 za shotgun, mabomu ya milipuko yaliyotengenezwa kienyeji matatu, vipande vidogo vya nondo 42, fyuzi zilizotegwa na fyuzi zilizotupu 56.

Kamanda Ibrahimu alisema vitu vingine vilivyokamatwa ni milipuko ya mafuta mitatu, silcon rubber zenye asilimia 100 ikiwa moja, nyaya tatu za milipuko, bunduki mbili zilizotengenezwa kienyeji na bunduki moja aina ya rifle.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!