WATANZANIA wameelezwa kuwa nchi yao itaendelea kuwa na amani huku maslahi ya taifa yakilindwa, endapo vyombo vya habari vya ndani vitafanya kazi yake kwa kuzingatia maadili na mipaka ya uhuru wa habari.
Aidha, wameshauriwa kutochukulia uwepo wa sheria za vyombo vya habari na hitaji la kuwa na mipaka katika kusambaza habari kuwa ni kuwanyima wanahabari uhuru wa kufanya kazi , kwa sababu vinawaepusha na uchochezi wa migogoro inayoepukika.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Zambia inayohusika na masuala ya Habari na Utangazaji, Kabinga Pande alisema hayo Dar es Salaam jana wakati kamati yake ya wajumbe tisa ilipoitembelea Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoshughulika na Huduma za Jamii.
Kamati ya Huduma za Jamii inaongozwa na Mwenyekiti, Said Mtanda aliyeunga mkono maelezo ya Pande kwa kusema, “Duniani kote hakuna uhuru wa vyombo vya habari usio na mipaka”.
Kutokana na maelezo ya Pande, uhuru wa vyombo vya habari uliopitiliza umekuwa chanzo kikubwa cha migogoro katika baadhi ya nchi za Bara la Afrika, hivyo, haupaswi kupendelewa sana.
Alisema, imekwishashuhudiwa watu wakiuana katika nchi mbalimbali kwenye Bara hilo la Afrika kwa sababu redio zao za kijamii zimetumika vibaya kutangaza habari zenye uchochezi, jambo linalochukuliwa kama fundisho na tahadhari kwa wananchi, hususan wanahabari kwenye nchi ambazo madhara kama hayo hayajatokea.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante Gabriel alisema wanahabari wa Tanzania wana uhuru wenye mipaka wa kuandika na kutangaza habari kwa sababu, hawalazimishwi waandike nini bali wanaongozwa watangaze na kuandika vipi wasivuruge amani.
No comments:
Post a Comment