Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limesema majina ya wapiganaji wa Tanzania waliofariki dunia kwa kushambuliwa na waasi wa ADF huko Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) yatatajwa baada ya miili hiyo kuwasili nchini.
Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja alisema jana kuwa kwa sasa wanasubiri maelekezo na taratibu za kuleta miili hiyo zikamilike.
Masanja aliwatoa hofu Watanzania kuhusu usalama wa askari wake walioko DRC, wanaoshiriki operesheni ya kulinda amani chini ya vikosi maalumu vya Umoja wa Mataifa.
Meja Masanja alisema kikundi cha wanajeshi 46 ambao ni walinzi wa amani kilisafiri kwa helikopta kutoka Mji wa Abialose kuelekea Mavivi na baada ya kufika walikwenda Mayimoya kwa gari. “Wakiwa njiani walishambuliwa na ADF kwa silaha za kivita na gari moja kuteketezwa na kusababisha vifo vya askari wetu na wengine 16 kujeruhiwa,” alisema.
Tukio hilo linafanya idadi ya wanajeshi wa Tanzania waliouawa nchini humo kufikia watatu baada ya askari mwingine, Khatibu Mshindo kuuawa Agosti 2013 katika shambulio la bomu lililofanywa na waasi wa kikundi cha M23 kwenye Mji wa Goma ulioko Mashariki mwa DRC.
Msemaji wa Mpango wa Kulinda Amani kutoka Umoja wa Mataifa, DRC, Felix Basse alikaririwa na Shirika la Habari la AFP akisema mashambulizi ya juzi yalifanyika katika Kijiji cha Kikiki kilichoko kilomita 37, Kaskazini-Mashariki mwa mji wa Kivu.
Habari nyingine zilizopatikana jana, zilisema kuwa askari wa Tanzania wameingia msituni kusaka waasi wa Uganda wa ADF walioshiriki mauaji hayo. Msemaji wa Misheni ya Kulinda Amani DRC, Monusco, Kanali Felix Basse alisema Umoja wa Mataifa umeongeza vikosi vya ulinzi eneo lililofanyika mauaji hayo.
“Tumepeleka askari zaidi eneo la Beni baada ya shambulio lile,” alisema Kanali Basse na kuongeza:
“Ni lazima kuendelea na mapigano haya... Nitazungumza na Waziri wa Ulinzi wa Tanzania (Dk Hussein Mwinyi), Dar es Salaam kumweleza hali ilivyokuwa na nini kinafanyika,” alisema Kanali Basse.
Hata hivyo, alisema UN haitakubali kuona suala hilo likijitokeza tena na tayari vikosi vimeongezwa katika eneo lilipotokea mauaji hayo yaliyoacha askari wengine 13 kujeruhiwa.
Baraza la Usalama lalaani
Wanachama wa Baraza la Usalama la UN, wamelaani mauaji hayo wakisema hatua hiyo inazorotesha jitihada za kuleta amani Mashariki mwa DRC
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment