Friday 8 May 2015

WAZAZI KUWENI KARIBU NA WATOTO WENU WASIHAMIE KUSIKOFAA


SITAKI kuamini nilichokisikia kuhusu kijana wa Kitanzania, Rashid Charles Mberesero (20) kutuhumiwa kuhusika katika mauaji ya watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya, Februari 2, mwaka huu.

Kutokana na taarifa zilizosambaa kwenye vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, na kwenye mitandao ya jamii, zikimtambulisha kijana huyo wa kidato cha tano kuwa ni Mtanzania, nyoyo za wengi zimestushwa.
Hata hivyo, lengo la waraka huu, si kueleza namna tulivyostushwa, kuhuzunishwa na pengine kuchukizwa na kusikia tunayoyasikia, ingawa vyombo vya usalama vinaendelea kufanya kazi yake kupata ukweli kamili.
Bali, kusudio ni kuwahamasisha wazazi, walezi, ndugu, jamaa na marafiki wa watoto wetu, wawe ndio kimbilio lao kuu, wawapo na furaha na hata wanapopata huzuni au kuwa na mambo yanayowasumbua.
Nasema hivyo kutokana na nilichokisoma na kukisikia katika vyombo hivyo vya habari, kuhusu mlolongo wa maisha ya kijana huyo, ambaye kwa sasa anashikiliwa na Polisi nchini Kenya kwa mahojiano na taratibu nyingine za kisheria.
Kwa mujibu wa maelezo ya baba mzazi wa kijana huyo, Charles Temba kwa vyombo mbalimbali vya habari, likiwemo Shirika la Habari la Uingereza (BBC), hakuwahi kuwa karibu na mwanawe huyo tangu azaliwe hadi mwaka jana, alipotambulishwa kwake na mama mzazi wa mtoto huyo, aitwaye Fatma Ali.
Mzee huyo alieleza kuwa baada ya kutambulishwa, alimkubali na kumsihi abadili dini zaidi ya mara tatu, jambo ambalo kijana huyo alilipinga na kuendelea kuwa Muislamu.
Kutokana na alichokisema kwa BBC, uhusiano wao uliishia hapo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kutofurahishwa na ushauri wa baba yake. Baba yake alinukuliwa akisema kuwa yeye ni Mkristo Mkatoliki, hivyo alipenda mwanawe huyo awe Mkristo pia.
Kwangu pia maneno hayo si tatizo, lakini narejea kuzungumzia ukaribu wa wazazi wote wawili kwa watoto wao. Natambua kuwa mama wa kijana huyo, alijitahidi kuhakikisha anakuza mtoto mzuri, ndio maana alikuwa akimsomesha, licha ya kutekeleza jukumu hilo kama mzazi pekee.
Lakini, ni lazima tuambiane ukweli. Kwa vyovyote vile, kama itathibitika moja kwa moja kuwa Mberesero alishiriki kuua watu wote hao kwa makusudi, mama mzazi niliyemsikia akieleza alichokitegemea kwa mwanawe kuwa ni kumpokea akiwa mwanasayansi mzuri, daktari au Injinia, ataumia sana.
Nasimama kama mzazi, pia kuzungumza haya, kwa sababu siamini endapo mama au baba anakuwa si gaidi, håalafu akasikia mwanawe anayemsumbukia awe na maisha mazuri amechipukia kwenye ugaidi, ni lazima atazizima kwa huzuni.
Tusubiri taarifa zaidi. Baada ya kusema hayo, napenda kuwaeleza wazazi kuwa wana wajibu wa kuhakikisha malezi ya watoto wao na kujenga ukaribu nao, kwa sababu wameshiriki kuwaleta duniani.
Itakuwa ni dhambi kuzaa na kutelekeza au kujifanya umesahau kuwa una mtoto mahali fulani, jambo linalowafanya wengine wakue wakiwa na msongo wa mawazo, kufikia kufanya mambo yasiyofaa na ya aibu kama hayo.
Chonde wazazi, walezi na jamaa wa watoto wetu, tuwape nafasi kusikia mawazo yao, tuwaoneshe upendo ili tuweze kuwarudi wanapoanza kwenda kombo.
Tunao watoto wengi mitaani, wengine wana wazazi, wengine ni yatima, lakini baadhi ya wenye wazazi wamekuwa wakitaja sababu za kutoroka nyumbani , shuleni na kuhamia mitaani kuwa ni pamoja na kunyanyaswa na wazazi au walezi, kubaguliwa na kupewa adhabu zilizopitiliza.
Wengine wanahamia kusikofaa kwa sababu ya kushawishiwa na watu wasiowatakia mema. Sasa hebu tujiulize, sisi wazazi tufanyeje ili tuwavute karibu wasikimbilie kusikofaa?

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!