GAZETI hili jana lilichapisha habari yenye kichwa cha habari ‘RC: Wakamateni wanaokatiza masomo watoto.’ Anayetoa amri hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk Ibrahim Msengi.
Amri hiyo inafuatia taarifa iliyoonesha kiwango cha juu cha utoro katika shule mbalimbali mkoani humo, iliyowasilishwa mbele ya kikao cha wadau wa elimu, kilichokuwa kinafanya tathmini ya maendeleo ya elimu.
Ripoti hiyo inaonesha zaidi ya asilimia 47 ya wanafunzi katika shule mbalimbali mkoani humo, wanakatiza masomo yao kutokana na sababu lukuki ikiwa ni pamoja na ujauzito, kutumikishwa mashambani na kuchunga mifugo kwa ujira mdogo.
Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Ernest Hinju alikiri kuwepo kwa kiwango hicho kikubwa cha utoro katika shule za msingi na sekondari, changamoto ambayo anasema inasababishwa na wazazi na walezi ambao huwashawishi watoto wao wasiende shule au wafanye vibaya mitihani yao kuhitimu shule ya msingi ili wasichaguliwe kwenda sekondari.
Hatua hii inalenga kujipatia nguvu kazi rahisi ya shughuli za kilimo au kuchunga mifugo. Tunaungana na Dk Msengi kwamba wazazi na walezi wa aina hii, wasakwe na kufikishwa mahakamani ili waweze kupata kile kinachowastahili kwa kuwakosesha watoto hao wa Kitanzania elimu ambayo ni ufunguo wa maisha yao.
Habari za aina hii za wazazi na walezi kufanya vituko kama hivi, zinaendelea kumiminika kutoka mikoa mingine pia, jambo ambao linadhihirisha wazi kuwa tatizo hili ni kubwa na halina budi kuchukuliwa kwa uzito wake katika ngazi zote katika jamii yetu.
Ni muhimu pia kukumbushana kwamba hivi sasa dunia hii ipo katika karne ya sayansi na teknolojia, ambayo kuipata kwake hakuna ujanja mwingine nje ya kupitia mfumo wa elimu, unaotambulika na kufahamika nchini na duniani kwa ujumla wake.
Kuwashawishi watoto wetu kuachana na shule kwa sababu yoyote ile wakiwa katika ngazi hiyo ya elimu ya msingi na sekondari, pia kunakaribisha tatizo lingine la kuwafanyisha kazi watoto kinyume na malezi ya watoto.
Hakuna ubishi kwamba hawatakiwi kufanyishwa kazi na kupewa ujira wa kiasi chochote kile, kwani ni kinyume na haki zao za msingi za malezi bora.
Wakati viongozi wa serikali wanatoa ushauri wa kuwafikisha mahakamani wazazi na walezi, wanaoendekeza tabia hii potofu dhidi ya watoto wao, tunapenda kutoa wito wa kuwepo na mshikamano katika kukabiliana na tatizo hili.
Hapa tunapendekeza kuwepo na mkakati wa makusudi wa kuhamasisha wananchi kupitia majukwaa ya kisiasa, huduma za jamii, sanaa na maonesho na mashirika na taasisi mbalimbali za dini, kufanya wazazi na walezi hao kuona umuhimu wa kupeleka watoto shule kwanza kabla ya hatua nyingine yoyote ya kuwapatia namna ya kujitafutia maisha yao wenyewe.
Kumnyima mtoto elimu ni sawa na kumnyang’anya ufunguo wake wa maisha na hatimaye atashindwa kupambana vyema na vita dhidi ya maradhi, ujinga na umasikini. Hili tulikatae kwa nguvu zote.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment